Jadon Sancho yupo tayari kusubiri hadi Januari kutafuta klabu sahihi
Hatma ya Jadon Sancho bado haijajulikana
Jadon Sancho, mshambuliaji mwenye kipaji ambaye kwa sasa yupo huru baada ya kuondoka Manchester United, ameamua kuwa na subira katika kutafuta changamoto yake mpya. Mchezaji huyu wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 26, yupo tayari kusubiri hadi dirisha dogo la usajili la Januari ikiwa hatapata ofa inayomridhisha kwa sasa.
Baada ya msimu uliopita kucheza kwa mkopo katika klabu ya Aston Villa akicheza michezo 39, Sancho amekuwa akitafuta klabu mpya itakayompa nafasi ya kuendeleza soka lake. Hata hivyo, mchakato huo umekuwa mgumu kuliko ilivyotarajiwa licha ya kuwepo kwa mazungumzo na timu mbalimbali.
Ofa za kila pembe ya dunia
Taarifa zinaeleza kuwa Sancho amekuwa na mazungumzo na klabu nyingi kutoka maeneo tofauti duniani. Hizi ni pamoja na timu za ligi mbalimbali barani Ulaya, Saudi Arabia, Marekani (MLS), pamoja na ofa za kuvutia kutoka Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Licha ya uvumi mwingi uliokuwa ukimhusisha na klabu ya Krasnodar ya nchini Russia, imebainika kuwa ofa hiyo haikuwahi kuwa sehemu ya mipango yake wala haikuja kutoka upande wake. Mazungumzo hayo yaliyoanzishwa na watu wa kati hayakupata baraka zozote kutoka kwa mchezaji huyo.
Noto ya kurudi Borussia Dortmund
Imefahamika kuwa Sancho alikuwa na shauku kubwa ya kurejea Borussia Dortmund, klabu ambayo ilimfanya kuwa nyota mkubwa kabla ya kuhamia Manchester United. Hata hivyo, mlango huo unaonekana kuwa umefungwa kwa sasa.
Klabu hiyo ya Bundesliga imemleta kinda wa Arsenal, Ethan Nwaneri kwa mkopo, jambo linalofanya nafasi ya Sancho kuzibwa kwa sasa. Ingawa kocha Niko Kovac anatajwa kuwa shabiki mkubwa wa uwezo wa Sancho, uongozi wa Dortmund hauna mpango wa kumrejesha mshambuliaji huyo wakati huu.
Subira kwa ajili ya mradi sahihi
Sancho kwa sasa anafanya mazoezi na klabu moja ya ligi za chini jijini Manchester ili kudumisha utimamu wa mwili. Lengo lake kuu si kupata klabu ya haraka, bali kupata mradi wa soka utakaomsaidia kufufua kiwango chake.
Klabu ya Como inayofundishwa na Cesc Fabregas pia ilitajwa kufuatilia uwezekano wa kumsajili, lakini mpaka sasa hakuna hatua kubwa iliyopigwa. Kwa hali hii, ni wazi kuwa Sancho yupo tayari kuvumilia mpaka Januari ili afanye uamuzi sahihi utakaokuwa na manufaa kwa kazi yake ya soka.