Jan Paul van Hecke apata wakati mgumu Tottenham, wachambuzi watabiri 'kushuka daraja'
Uchezaji wa Van Hecke wazua maswali
Beki mpya wa Tottenham Hotspur, Jan Paul van Hecke, amekumbwa na wimbi la ukosoaji baada ya kuonyesha kiwango hafifu katika mchezo ambao Spurs walipoteza kwa 3-2 dhidi ya Aston Villa. Usajili wa mchezaji huyu raia wa Uholanzi kutoka Brighton kwa kiasi cha pauni milioni 52, ulikuwa unatarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi ya klabu hiyo, lakini hadi sasa mambo hayajawa shwari.
Gwiji wa Nottingham Forest, Stuart Pearce, ambaye alikuwa mchambuzi katika mchezo huo, hakuwa na maneno ya kuficha hisia zake baada ya beki huyo kupoteza mpira kwa urahisi dhidi ya Nicolas Jackson wa Aston Villa.
“Kweli alijiuza vibaya. Je, huo ndio ulinzi wa thamani ya pauni milioni 52?” Pearce alihoji huku akionyesha kusikitishwa na namna Van Hecke alivyocheza.
Pearce aliongeza kuwa tangu usajili huo ufanyike kwa pesa nyingi, alikuwa na mashaka na uwezo wa mchezaji huyo, na utendaji wake uwanjani katika mchezo huo umeendelea kuibua maswali hayo hayo.
‘Anacheza kama mtu mwenye zege’
Si Pearce pekee aliyemkosoa mlinzi huyo. Mchezaji wa zamani wa Tottenham, Jamie O’Hara, naye hakubaki nyuma. Katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), O’Hara alimchambua mchezaji huyo kwa lugha kali:
“Van Hecke anaonekana kama anacheza akiwa amevaa zege miguuni mwake,” alisema O’Hara.
Tottenham kwenye hali mbaya?
Kiwango cha timu kwa ujumla kimezua hofu kubwa kwa O’Hara, ambaye haoni mwanga wowote kwa klabu hiyo ya London. Katika mahojiano yake, alionyesha kuchoshwa na hali ya timu, akisema kuwa Spurs hawana mpango wowote uwanjani.
“Siamini jinsi tulivyo wabovu. Nini kimetokea kwa klabu hii? Hatuna kiungo, hakuna mapambano kwenye timu hii hata kidogo. Wachezaji wanatembea tu uwanjani,” O’Hara alilalamika.
Kutokana na hali hiyo, O’Hara alifikia hatua ya kutoa utabiri mzito kuhusu mustakabali wa Tottenham kwenye Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu:
“Sisi ni timu laini zaidi kwenye Ligi Kuu, tunakwenda kushuka daraja. Nikiangalia timu nyingine, zote ni bora kuliko sisi hivi sasa. Tumetumia pauni milioni 400 lakini bado tuko kwenye hatari kubwa ya kushuka.”
Kwa sasa, shinikizo linazidi kuongezeka kwa wachezaji na benchi la ufundi la Tottenham kuhakikisha wanabadilisha matokeo haya kabla mambo hayajawa mabaya zaidi kwenye ligi.