JJ Gabriel huenda akasalia Manchester United baada ya Barcelona kuweka ngumu
Mustakabali wa JJ Gabriel bado haujajulikana
Kinda anayesumbua vichwa vingi barani Ulaya, JJ Gabriel, huenda akajikuta akibadili uamuzi wake wa kuondoka Manchester United. Hali hii inakuja kufuatia taarifa kwamba klabu kubwa ya FC Barcelona imefunga mlango wa kumsajili kinda huyo mwenye umri wa miaka 15 kwa sasa.
Awali, Gabriel aliripotiwa kuwa mbioni kutimka Old Trafford baada ya kutokea kutoelewana kati ya familia yake na uongozi wa klabu hiyo. Hata hivyo, inaonekana ndoto yake ya kujiunga na miamba ya soka nchini Hispania, hususan Barcelona au Real Madrid, inaweza kukumbwa na changamoto kubwa.
Barcelona wagomea dili hilo
Mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, Deco, tayari ameshatoa msimamo wa klabu hiyo kuhusu tetesi za kumsajili Gabriel. Kwa mujibu wa wachambuzi wa soka barani Ulaya, Barcelona wametoa majibu ya “hapana” kwa hatua yoyote ya kumsajili kinda huyo kwa sasa.
Akizungumzia hali hiyo, mchambuzi Kevin Hatchard alibainisha kuwa sheria za usajili za FIFA zinazuia wachezaji wa umri wa Gabriel kufanya uhamisho wa kimataifa kabla ya kufikisha miaka 16. Hii inamaanisha kuwa hata kama klabu hizo zingekuwa na nia, kuna vizuizi vya kisheria vinavyomfanya kinda huyo kubaki Manchester United angalau hadi atakapofikisha umri huo mwezi ujao.
“Kwa hatua hii, hawawezi kuonekana wakifanya jaribio la kumsajili mchezaji mdogo kiasi hicho… ni lazima wafuate taratibu,” alieleza Hatchard.
Je, atabaki Manchester United?
Ingawa mchezaji huyo anaonekana kuvutiwa zaidi na ligi ya LaLiga, ukweli ni kwamba Manchester United haionekani kuwa tayari kuvunja mkataba wake kirahisi. Hali hii inamfanya Gabriel na familia yake kulazimika kutafakari kwa kina kuhusu hatua inayofuata.
Hatchard aliongeza kuwa ni muhimu sana kwa kinda huyo kufanya maamuzi sahihi ili asije akapotea kwenye ramani ya soka. Alitoa mfano wa Jamal Musiala aliyesajiliwa na Bayern Munich kutoka Chelsea akiwa na umri wa miaka 16, akisema kuwa makuzi sahihi ndiyo siri ya mafanikio kwa wachezaji wachanga.
“Kama utafanya uamuzi mbaya katika umri huu, inaweza kuwa vigumu sana kwa sababu kwenye soka unaweza kusahaulika haraka. Ni muhimu kupata sehemu sahihi ya kukuza kipaji chako,” alisisitiza Hatchard.
Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwa hatua atakazochukua Gabriel atakapofikisha umri wa miaka 16 mwezi ujao, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa yeye kubaki Old Trafford au kusubiri ofa nyingine tofauti na alivyotarajia.