Skip to content

Jose Mourinho tayari kumuuza Eduardo Camavinga, Chelsea wajipanga

SokaNews
Updated: Published: Jumatano, 24 Juni 2026 · 2 min read
chelsea realmadrid eduardocamavinga josemourinho usajili premierleague
Jose Mourinho tayari kumuuza Eduardo Camavinga, Chelsea wajipanga

Mourinho afungua mlango kwa Camavinga kuondoka

Klabu ya Chelsea imepata mwanga mpya katika jitihada zao za kumsaka kiungo wa Real Madrid, Eduardo Camavinga. Taarifa kutoka nchini Hispania zinaeleza kuwa kocha mpya wa klabu hiyo ya jijini Madrid, Jose Mourinho, yuko tayari kusikiliza ofa kwa ajili ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 23.

Camavinga, ambaye amekuwa na mafanikio makubwa tangu ajiunge na Madrid ikiwemo kutwaa mataji ya LaLiga na Ligi ya Mabingwa Ulaya, amepitia kipindi kigumu katika misimu miwili iliyopita kutokana na majeraha ya mara kwa mara. Hali hiyo ilipelekea pia jina lake kukosekana kwenye kikosi cha Ufaransa kilichopo nchini kwa ajili ya Kombe la Dunia 2026.

Chelsea na vigogo wengine vitani

Si Chelsea pekee inayomnyatia staa huyu. Ripoti zinasema kuwa klabu za Manchester United, Liverpool na Juventus pia zimepiga hodi Real Madrid kuulizia hali ya kiungo huyo. Chelsea, ambao kwa sasa wananolewa na kocha Xabi Alonso, wanaonekana kuwa na nia ya dhati ya kuimarisha eneo lao la kiungo kwa mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi, ikiwemo beki ya kushoto.

Ingawa thamani yake ya sokoni imeshuka kutoka Euro milioni 100 hadi Euro milioni 50 kutokana na changamoto za majeraha, Camavinga bado ana mkataba mnono hadi mwaka 2029, wenye kipengele cha kuvunja mkataba kinachofikia Euro bilioni 1.

Msimamo wa mchezaji mwenyewe

Licha ya Mourinho kuonekana tayari kumuuza, duru za karibu na kiungo huyo zinaeleza kuwa Camavinga bado anatamani kupambania nafasi yake ndani ya Santiago Bernabeu. Inaelezwa kuwa kwa mchezaji huyo, kuondoka Madrid katika kipindi hiki ni jambo lisilowezekana.

Awali, mchambuzi wa masuala ya usajili Fabrizio Romano alieleza kuwa mchezaji huyo ana nia ya dhati ya kufanikiwa Madrid licha ya msimu uliopita kuwa mbaya kwake. Alisema:

“Camavinga hataki kukata tamaa. Anaelewa kuwa msimu huu ulikuwa mgumu kwake binafsi, katikati ya majeraha na bahati mbaya, lakini yuko tayari kuanza upya na kuonyesha uwezo wake. Anataka kuwa sehemu ya mradi wa Real Madrid.”

Sasa bado inasubiriwa kuona kama Chelsea au klabu nyingine zitawasilisha ofa kubwa itakayoshawishi uongozi wa Real Madrid na Mourinho kubadili msimamo wao na kumruhusu mchezaji huyo kuondoka.