Skip to content

Joshua Zirkzee afungua mlango kuondoka Manchester United, Juventus wajipanga

SokaNews
Updated: Published: Jumatano, 22 Julai 2026 · 2 min read
manchesterunited joshuazirkzee juventus lisandromartinez usajili seriea
Joshua Zirkzee afungua mlango kuondoka Manchester United, Juventus wajipanga

Zirkzee anatazamiwa kurejea Italia

Mshambuliaji wa Manchester United, Joshua Zirkzee, ameripotiwa kuwa tayari kuondoka Old Trafford katika dirisha hili la usajili ili kutafuta changamoto mpya nchini Italia, ambako klabu ya Juventus inaonekana kuwa na nia ya dhati kumsajili.

Mholanzi huyo alijiunga na United wakati wa utawala wa Erik ten Hag, lakini tangu kuondoka kwa kocha huyo, mambo hayakuwa mepesi kwa mshambuliaji huyo. Katika kipindi chake cha misimu miwili Old Trafford, Zirkzee amefanikiwa kuanza michezo 19 pekee ya Ligi Kuu ya Uingereza na kufunga mabao matano, jambo lililozua mjadala kuhusu mustakabali wake.

Ushauri wa Ruud Gullit

Mkongwe wa soka nchini Uholanzi, Ruud Gullit, hivi karibuni alimshauri mwananchi mwenzake huyo kuwa alifanya uamuzi mbaya kujiunga na Manchester United. Gullit anaamini kuwa Zirkzee alipaswa kubaki nchini Italia, akihusisha hali ya sasa ya kikosi cha United na changamoto anazokutana nazo mchezaji huyo.

“Joshua Zirkzee alifanya kosa kwenda Manchester United. Alipaswa kubaki Italia. Alipofika pale, klabu ilikuwa katika hali ya taharuki na wakati haukuwa sahihi kwake. Natumai atarejea Italia kwani ligi hiyo inamfaa zaidi,” alisema Gullit.

Ripoti kutoka gazeti la Gazzetta Dello Sport zinasema kuwa Juventus wamekuwa wakifanya mawasiliano ya karibu na wawakilishi wa Zirkzee. Ofisa wa soka wa Juventus, Ricky Massara, anatajwa kuwa amekuwa akitumia muda mwingi kujaribu kukamilisha dili hili la mshambuliaji huyo sambamba na Randal Kolo Muani wa Paris Saint-Germain.

Lisandro Martinez naye hatarini?

Wakati Zirkzee akihusishwa na kuondoka, taarifa nyingine zinambeba beki kisiki Lisandro Martinez. Mchambuzi wa mambo ya soka na aliyewahi kuwa mkuu wa skauti wa Manchester United, Mick Brown, anaamini klabu hiyo inaweza kufikiria kumuachia beki huyo ikiwa matatizo yake ya majeraha yataendelea kuwa sugu.

Martinez amekuwa na changamoto kubwa ya majeraha yaliyomfanya akose michezo mingi muhimu msimu uliopita. Brown anaeleza kuwa licha ya ubora wake uwanjani, hali ya kutopatikana mara kwa mara ni jambo linaloisumbua klabu.

“Ni pigo kubwa kuona Martinez anapata jeraha lingine. Ni mchezaji muhimu anapokuwa fiti, lakini sifa hizo hazina faida kama kila wakati yupo jukwaani akiuguza majeraha. Ikiwa kutakuwa na ishara kuwa hali hii itaendelea, sioni ajabu wakiamua kupunguza hasara na kumuuza,” alisema Brown.

Kwa sasa, mashabiki wa United wanabaki kusubiri kuona ni maamuzi gani yatafikiwa na uongozi wa klabu hiyo kuhusiana na nyota hawa wawili katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu.