Skip to content

Joshua Zirkzee mbioni kuondoka Man Utd, Fiorentina yaweka ofa mezani

SokaNews
Updated: Published: Alhamisi, 27 Agosti 2026 · 2 min read
manchesterunited joshuazirkzee fiorentina usajili premierleague igormatanovic
Joshua Zirkzee mbioni kuondoka Man Utd, Fiorentina yaweka ofa mezani

Zirkzee kuondoka Old Trafford?

Klabu ya Manchester United ipo katika hatua za mwisho za kuachana na mshambuliaji wao, Joshua Zirkzee, ambaye sasa anatajwa kuwa mbioni kujiunga na klabu ya Fiorentina ya nchini Italia.

Taarifa kutoka kwa mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, zimethibitisha kuwa tayari klabu hiyo ya Serie A imewasilisha ofa rasmi kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo wa Uholanzi. Inasemekana kuwa ofa hiyo ni ya mkopo kwa ada ya Euro milioni 5, huku kukiwa na kipengele cha kumnunua jumla baada ya msimu kumalizika.

Uwanja wa usajili unanoga

Katika dirisha hili la usajili, Manchester United imekuwa ikifanya marekebisho makubwa kwenye kikosi chao, wakijikita zaidi kuimarisha safu ya kiungo kwa kuwasajili wachezaji kama Carlos Baleba, Youri Tielemans, na Andrey Santos. Hata hivyo, inaonekana klabu hiyo haijatosheka na bado inatazama uwezekano wa kuongeza nguvu katika nafasi nyingine.

Kulingana na ripoti za mwandishi Ben Jacobs, kuondoka kwa Zirkzee kutazilazimisha klabu hiyo kuharakisha jitihada za kusaka mshambuliaji mwingine mpya kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Ingawa kipaumbele chao cha sasa kinaonekana kuwa ni beki wa kushoto, nafasi ya ‘Namba 9’ nayo imekuwa ikifuatiliwa kwa ukaribu.

Nani atachukua nafasi yake?

Kufuatia kuingia katika hatua za lala salama za kumpoteza Zirkzee, Manchester United sasa inatajwa kuingia kwenye ushindani na Tottenham Hotspur kwa ajili ya kumsaka mshambuliaji mwenye umri wa miaka 23, Igor Matanovic, anayekipiga katika klabu ya Freiburg.

Wakati huo huo, wapo wachambuzi wanaoamini kuwa United ilipoteza nafasi nzuri ya kumsajili Ollie Watkins, ambaye alikuwa chaguo bora kwa ajili ya kuongoza safu ya ushambuliaji.

Akizungumzia suala hilo, mchezaji wa zamani wa United, Lee Sharpe, alitoa maoni yake:

“Nafikiri angekuwa usajili bora. Anajua kutunza mpira, ana kasi, anafunga magoli nafikiri yupo katika umri ambao angeweza kuja na kutotishwa na changamoto ya Manchester United na matarajio waliyonayo kwa namba tisa.”

Kwa sasa, mashabiki wa United wanaendelea kusubiri kuona nani atakuwa chaguo la mwisho la klabu hiyo, huku dirisha la usajili likielekea ukingoni.