Skip to content

Joto kali Miami lahatarisha mchezo wa robo fainali kati ya England na Norway

SokaNews
Updated: Published: Jumamosi, 11 Julai 2026 · 2 min read
kombeladunia2026 england norway erlinghaaland harrykane miami
Joto kali Miami lahatarisha mchezo wa robo fainali kati ya England na Norway

Joto kali lasababisha sintofahamu Miami

Safari ya England na Norway katika michuano ya Kombe la Dunia 2026 imegubikwa na taharuki baada ya taarifa kuibuka kuwa mchezo wao wa robo fainali uliopangwa kufanyika leo jijini Miami, huenda ukaahirishwa au kuchelewa kuanza kutokana na hali ya hewa ya joto kali.

Mchezo huo mkali umepangwa kupigwa katika uwanja wa Miami, lakini hali ya joto imefikia kiwango ambacho kimezua hofu kubwa kwa mamlaka husika. Kwa mujibu wa ripoti kutoka nchini humo, joto linakadiriwa kufikia nyuzi joto 29 hadi 32, huku hali halisi ya joto (realfeel) ikitabiriwa kupanda hadi kufikia nyuzi joto 44 wakati mchezo huo ukitarajiwa kuanza.

Mamlaka ya jiji la Miami imetoa tahadhari kubwa ya kiafya kwa wakazi wake, ikisisitiza umuhimu wa watu kukaa kwenye maeneo yenye viyoyozi, kunywa maji mengi, na kupunguza shughuli za nje wakati huu wa jua kali. Kwa mujibu wa miongozo ya chama cha wachezaji duniani (FIFPRO), michezo ya soka inashauriwa kucheleweshwa au kuahirishwa endapo joto la eneo husika litazidi nyuzi joto 28.

Haaland: Presha yote iko kwa England

Wakati hali ikiwa tete nje ya uwanja, ndani ya dimba macho yote yameelekezwa kwa washambuliaji wawili hatari zaidi duniani, Erling Haaland wa Norway na nahodha wa England, Harry Kane.

Akizungumza kabla ya mchezo huo, mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, alionekana kutaka kuhamishia presha yote kwa vijana wa Thomas Tuchel. Haaland alisisitiza kuwa England ndio wanaobeba jukumu kubwa la kushinda mchezo huu.

“Ndiyo, bila shaka. Nadhani kuna timu zinazopewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda, na England ni moja ya hizo. Nadhani nyinyi waandishi mnapaswa kuweka presha yote kwa wavulana wa England. Mashabiki wanapaswa kuwa na imani ya kusonga mbele, bila shaka. Ni England,” alisema Haaland.

Vita ya wafungaji bora

Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, si tu kwa timu bali pia kwa wachezaji binafsi wanaowania kiatu cha dhahabu. Haaland amekuwa katika kiwango bora kabisa akiwa amefunga mabao saba katika michezo minne aliyoichezea Norway kwenye michuano hii.

Kwa upande mwingine, Harry Kane ambaye msimu uliopita alitwaa ubingwa wa Bundesliga akiwa na Bayern Munich, naye hajaachwa nyuma. Kane amefikisha mabao sita katika michezo mitano aliyoichezea timu yake ya taifa ya England mpaka sasa.

Mashabiki wa soka kote ulimwenguni wanaendelea kusubiri taarifa rasmi kutoka kwa waandaaji wa michuano hii, kuhusu hatima ya mchezo huu ambao unatajwa kuwa moja ya mechi ngumu zaidi katika hatua hii ya robo fainali.