Gary Lineker aibua hofu kwa nyota wa England, Elliot Anderson, kuelekea nusu fainali dhidi ya Argentina
Hofu ya Lineker kwa kiungo wa England
Gwiji wa soka nchini England, Gary Lineker, ameweka wazi wasiwasi wake kuhusu kiungo machachari wa Manchester City, Elliot Anderson, kuelekea pambano kubwa la nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya mabingwa watetezi, Argentina.
Ingawa Anderson amekuwa na mchango mkubwa katika kuisaidia England kutinga nusu fainali baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norway katika mchezo uliomalizika kwa muda wa ziada, Lineker anaona kuna changamoto ndogo inayoweza kuigharimu timu hiyo dhidi ya wapinzani wakubwa kama Argentina.
Kiwango bora lakini chenye changamoto
Akizungumza kwenye kipindi cha The Rest is Football, Lineker alimsifu Anderson kwa uwezo wake mkubwa wa kupiga pasi na juhudi zake uwanjani kwa dakika zote 120 dhidi ya Norway. Hata hivyo, alibainisha jambo moja ambalo linaweza kuleta madhara.
“Elliot Anderson alikuwa mzuri sana. Pasi zake na zile za pembeni zilikuwa safi. Alikimbia sana kwa dakika zote 120. Kitu kimoja ninachoweza kusema ni kwamba wakati mwingine anapenda kupanda sana mapema. Ikiwa una wachezaji kama Jude Bellingham na Declan Rice mbele yake, mara nyingine tunabaki wazi sana mbele ya mabeki wetu wanne.”
Lineker aliongeza kuwa ingawa Anderson ni mchezaji mahiri, wasiwasi huo unatokana na ukweli kwamba Argentina ni timu tofauti kabisa na Norway, na makosa madogo yanaweza kuadhibiwa.
Ushauri wa Micah Richards
Naye mchambuzi Micah Richards amemuunga mkono Lineker, akisisitiza kuwa Anderson anahitaji nidhamu zaidi ya kimchezo ili kucheza vyema katika nafasi hiyo ya kiungo.
Richards anaamini kuwa Anderson ni kiungo namba nane wa asili na si namba sita. Alisema:
“Yeye ana uwezo mkubwa wa kiufundi, anapiga pasi safi na ana nguvu nyingi. Anataka kuhusika katika kila eneo. Lazima awe na nidhamu zaidi. Ukicheza dhidi ya timu kama Ufaransa na mchezaji kama Michael Olise akicheza namba 10, utaumia haraka sana.”
Richards alihitimisha kwa kusema kuwa kama Anderson akirekebisha madogo hayo ya kiufundi, anaweza kufika mbali sana, akibainisha kuwa ndiyo sababu Manchester City walimsajili ili kuleta nguvu mpya kwenye kikosi chao.
England sasa inajipanga kwa ajili ya mchezo huo wa nusu fainali huku mashabiki wakiwa na matumaini ya kuona timu hiyo ikikabiliana na Argentina kwa umakini mkubwa ili kufuzu fainali ya michuano hii mikubwa duniani.