Lineker na Shearer wamshambulia Michael Carrick kwa kutomtumia Sesko
Uamuzi wa Carrick wazua mjadala
Magwiji wa soka wa Uingereza, Gary Lineker na Alan Shearer, wameibua mjadala mzito kuhusu namna kocha Michael Carrick anavyopanga safu yake ya ushambuliaji katika kikosi cha Manchester United. Mjadala huu umekuja kufuatia matokeo mabaya ya kichapo cha 1-0 walichopata dhidi ya wapinzani wao Manchester City mwishoni mwa juma.
Katika mchezo huo, United ilionekana kukosa makali licha ya mpinzani wao kubaki pungufu baada ya Phil Foden kuonyeshwa kadi nyekundu. Hata hivyo, wengi walitarajia kuona mabadiliko ya haraka kwenye safu ya ushambuliaji, lakini mshambuliaji matata Benjamin Sesko aliingia uwanjani dakika ya 67 pekee, muda ambao wachambuzi hao wanaona haukutosha.
Sesko anahitaji muda zaidi
Lineker, kupitia kipindi chake cha The Rest Is Football, alionyesha kushangazwa na uamuzi wa Carrick kumweka benchi mshambuliaji huyo ambaye amekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga anapopata nafasi.
“Unaanza kujiuliza kuhusu Manchester United. Unamuangalia Sesko yuko benchi. Ni jambo la kushangaza, amekuwa akifunga kwenye michezo mingine lakini bado hupati jibu kwa nini hapati nafasi ya kuanza. Ulikuwa unaangalia mchezo na kufikiri, ‘Kama unahitaji mtu kule mbele… kwanini usimuingize yule mtu mkubwa?’ na kweli aliingia lakini alichelewa sana,” alisema Lineker.
Kwa upande wake, Alan Shearer alikubaliana na mtazamo huo, akisisitiza kuwa Carrick alipaswa kumtumia Sesko mapema zaidi ili kuongeza presha kwenye ngome ya City.
“Angeweza kumpa muda zaidi Sesko. Nilikuwa nikisema, ‘Lazima amuingize!’ na niliona angeweza kumuingiza angalau dakika kumi kabla ya muda aliomuingiza,” aliongeza Shearer.
Changamoto kwenye safu ya ushambuliaji
Shearer pia aligusia utata wa ubora wa safu ya ushambuliaji ya United kwa ujumla. Ingawa klabu hiyo imefanya usajili kadhaa katika maeneo ya kiungo na mbele, gwiji huyo anaamini bado kuna pengo kubwa ukilinganisha na timu nyingine kubwa kwenye ligi.
“Kuna mazungumzo kuhusu namna walivyoimarisha safu ya mbele na kiungo, lakini hawakuimarisha ulinzi. Sijui kwa uhakika kama wako vizuri sana kule mbele pia. Nadhani wapo sawa tu, ni wa kawaida. Lakini ukilinganisha na timu nyingi kubwa…” alionya Shearer.
Katika mchezo huo dhidi ya City, United ilipiga mashuti matatu pekee yaliyolenga lango, huku wachezaji kama Matheus Cunha na Marcus Rashford wakishindwa kuleta madhara makubwa mbele ya goli. Hali hii imeacha maswali mengi kwa mashabiki na wachambuzi kama kikosi cha Carrick kitakuwa na uwezo wa kushindana katika kiwango cha juu msimu huu.