Liverpool kuingilia kati dili la Ousmane Diomande kwenda Nottingham Forest
Liverpool yavizia hatua ya Nottingham Forest
Klabu ya Liverpool imeripotiwa kuwa kwenye nafasi nzuri ya kumsajili beki kisiki wa Sporting Lisbon, Ousmane Diomande, kufuatia kuyumba kwa mazungumzo kati ya mchezaji huyo na Nottingham Forest.
Awali, Nottingham Forest walionekana kuwa mbioni kukamilisha usajili wa beki huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye amekuwa kwenye rada za vilabu vingi vikubwa barani Ulaya kwa kipindi kirefu. Hata hivyo, hali imebadilika ghafla katika siku za karibuni.
Mgogoro wa malipo waibua sintofahamu
Ripoti kutoka nchini Ureno kupitia chombo cha habari cha A Bola, zinaeleza kuwa licha ya pande zote mbili kuwa karibu kufikia muafaka mapema wiki hii, mazungumzo hayo yalikwama kutokana na kutokuelewana kuhusu utaratibu wa malipo.
Sporting Lisbon inatarajia kupokea kiasi cha Euro milioni 40 kama ada ya uhamisho, huku kukiwa na nyongeza za bonasi zinazoweza kufikisha dili hilo hadi Euro milioni 45. Aidha, klabu hiyo ya Ureno inataka sehemu ya faida itakayopatikana endapo mchezaji huyo atauzwa tena hapo baadaye.
Ingawa ada ilikubalika, mpangilio wa muda wa malipo ndiyo imekuwa kikwazo kikubwa kilichosababisha mchakato huo kusimama kwa sasa, jambo ambalo limetoa mwanya kwa vilabu vingine kuingia vitani.
Liverpool watajwa kuingilia kati
Liverpool, ambao kwa sasa wamejikita zaidi katika kuimarisha safu yao ya ushambuliaji, wanaelezwa kuwa wanaweza kubadilisha mwelekeo na kuingilia kati ili kumsajili beki huyo wa kimataifa wa Ivory Coast.
Mwandishi wa habari za michezo, Sebastien Vidal, amedokeza kupitia mitandao ya kijamii kuwa Liverpool inaweza kunufaika na kusuasua kwa dili la Nottingham Forest.
“Liverpool inaweza kunufaika na kufeli kwa mazungumzo kati ya Nottingham Forest na Sporting kwa ajili ya Ousmane Diomande. Beki huyo wa Ivory Coast mwenye thamani ya takriban Euro milioni 40, bado anapatikana na amekuwa kwenye rada za majogoo hao wa Anfield kwa muda mrefu huku wakitafuta kuimarisha safu yao ya ulinzi,” alisema Vidal.
Je, Liverpool inahitaji beki?
Ingawa taarifa nyingi zimekuwa zikiihusisha Liverpool na washambuliaji kama Bradley Barcola na Ibrahim Mbaye kutoka PSG, ukweli ni kwamba timu hiyo ina upungufu katika safu ya ulinzi. Majeruhi ya mara kwa mara yamefanya chaguzi za kocha kuwa chache katika eneo la kati la ulinzi (centre-back) pamoja na beki za pembeni.
Bado haijafahamika kama Liverpool wataamua rasmi kuingia sokoni kwa ajili ya beki, lakini uwezo wa Diomande kucheza kwa kiwango cha juu unawafanya kuwa washindani hatari kwa Nottingham Forest ambao kwa sasa wako kwenye wakati mgumu kukamilisha makubaliano yao.