Liverpool kupanga kumpa mkataba mpya kinda Rio Ngumoha
Liverpool wajipanga kumfunga Rio Ngumoha
Klabu ya Liverpool imeripotiwa kuwa kwenye hatua nzuri za kufikia makubaliano ya mkataba mpya na kinda wake matata, Rio Ngumoha. Kinda huyo amekuwa moja ya nyota walioonyesha kiwango kikubwa ndani ya klabu hiyo, jambo lililowafanya mabosi wa Anfield kuamua kumtathmini upya ili kumlinda na washawishi kutoka klabu nyingine.
Awali, kulikuwa na tetesi zilizomhusisha Ngumoha na mpango wa kutaka kuhamia Bayern Munich mapema katika dirisha hili la usajili. Hata hivyo, Liverpool imekuwa ikifanya kila liwezekanalo kukanusha taarifa hizo, huku mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, akisisitiza kuwa kijana huyo hayupo sokoni.
βRio Ngumoha hakuwa karibu kabisa kujiunga na Bayern Munich majira haya ya joto. Kwa Liverpool, yeye ni sehemu muhimu sana ya mradi wao wa sasa na wa baadaye,β alisema Romano.
Uboreshaji wa mkataba
Taarifa zinaeleza kuwa Liverpool sasa wapo tayari kutambua mchango na kukua kwa haraka kwa kinda huyo kwa kumpa mkataba wenye maslahi makubwa zaidi. Ikumbukwe kuwa alipojiunga na klabu hiyo, aliingia kwa mkataba wa miaka mitatu, ambao ndio uliokuwa wa juu zaidi kwa umri wake wakati huo.
Sasa, mabosi wa Liverpool wamejipanga kumpa nyongeza kubwa ya mshahara, huku pia mkataba mpya ukijumuisha vipengele vya bonasi kulingana na uchezaji wake, ikiwemo idadi ya mechi atakazocheza katika ngazi ya kimataifa. Hatua hii inaashiria imani kubwa ambayo klabu inayo kwa Ngumoha, ikimwona kama mchezaji atakayekuja kuwa nguzo muhimu kwenye timu ya wakubwa.
Hali ya Cody Gakpo
Katika tukio jingine linaloendelea ndani ya klabu hiyo, ripoti zinaonyesha kuwa mshambuliaji Cody Gakpo ameiambia Liverpool kuwa anatamani kuondoka na kujiunga na Tottenham Hotspur.
Inaelezwa kuwa wawakilishi wa Gakpo wameshafikia makubaliano binafsi na Tottenham, na tayari wameanza mazungumzo na uongozi wa Liverpool ili kuweka wazi nia ya mchezaji huyo kutaka kuondoka Anfield. Gakpo anaonekana kutokuwa na mipango ya muda mrefu ndani ya Liverpool, hatua inayoongeza uwezekano wa klabu hiyo kutafuta mbadala katika eneo la ushambuliaji.