Skip to content

Liverpool kunufaika na mvutano wa Chelsea na Monaco kuhusu Lamine Camara

SokaNews
Updated: Published: Jumamosi, 5 Septemba 2026 · 2 min read
liverpool chelsea monaco laminecamara usajili fabrizioromano
Liverpool kunufaika na mvutano wa Chelsea na Monaco kuhusu Lamine Camara

Mvutano wa Chelsea na Monaco kufungua njia kwa Liverpool

Klabu ya Liverpool inaweza kuwa imepta mwanga mpya katika azma yake ya kuimarisha safu ya kiungo, baada ya kutokea kwa mgogoro mkubwa kati ya Chelsea na Monaco kufuatia sakata la usajili wa Lamine Camara.

Katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili, Chelsea walikuwa wamefikia makubaliano ya kumsajili Camara huku mchezaji huyo akiwa tayari ameshaanza taratibu za vipimo vya afya. Hata hivyo, mambo yaliharibika dakika za mwisho baada ya Monaco kuvuta hisa na kusitisha makubaliano hayo ghafla.

Chelsea wamekasirishwa na Monaco

Mchambuzi wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amebainisha kuwa uongozi wa Chelsea umekasirishwa sana na kitendo hicho cha Monaco. Inasemekana kuwa hali hiyo imeharibu kabisa uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya klabu hizo mbili.

“Chelsea wamekasirika sana na wamefadhaika na Monaco, na hii inaelekea kuathiri uhusiano kati ya klabu hizi mbili, angalau kwa muda huu wa uongozi wa sasa,” alisema Romano kupitia chaneli yake ya YouTube.

Nafasi kwa Liverpool?

Romano anaamini kuwa kutokana na hali hiyo ya sintofahamu, ni vigumu kwa Chelsea na Monaco kufanya biashara yoyote ya usajili katika siku za usoni. Hii inatazamwa kama faida kwa Liverpool, ambayo hapo awali iliripotiwa kuonyesha nia ya kumtaka Camara.

Ingawa Chelsea walikuwa wameshaandaa nyaraka zote na kuzisaini na Monaco, kitendo cha Monaco kukataa kukamilisha dili hilo kimeacha makovu. Romano anaongeza kuwa ni vigumu kwa Chelsea kurejea tena kwa mchezaji huyo mwezi Januari kutokana na jinsi mambo yalivyoharibika.

“Hisia zangu ni kwamba vilabu hivi viwili havitafanya biashara kwa muda mrefu. Hii si hali ya kawaida ambapo Chelsea wanaweza kuwa na uhakika wa kurejea kwa mchezaji yuleyule mwezi Januari kutokana na yaliyotokea,” aliongeza Romano.

Kwa sasa, mashabiki wa Liverpool wanakaa mkao wa kula wakifuatilia hatua inayofuata, huku kukiwa na matumaini kuwa mvutano huu wa kimaslahi kati ya mahasimu wao wa Ligi Kuu ya England na klabu hiyo ya Ufaransa, unaweza kuwapa nafasi nzuri ya kumnasa kiungo huyo chipukizi katika madirisha yajayo ya usajili.