Liverpool kupewa nafasi ya kumsajili Bradley Barcola kutoka PSG
Liverpool yajipanga kumnasa Bradley Barcola
Klabu ya Liverpool imeonekana kupewa nafasi kubwa ya kufanikisha usajili wa winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, katika dirisha hili la usajili. Hatua hii inakuja wakati Liverpool ikitafuta mbadala wa muda mrefu wa gwiji wao Mohamed Salah, ambaye anahusishwa na kuondoka kuelekea Saudi Pro League au ligi ya Marekani (MLS).
Ingawa Liverpool tayari imefanikiwa kumsajili Victor Munoz kutoka Osasuna kwa ada ya Euro milioni 40, inaonekana kocha anaamini bado wanahitaji winga mwingine wa kiwango cha juu ili kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.
Barcola si ‘untouchable’ tena
Kwa muda mrefu, Barcola alionekana kama mchezaji ambaye hauziki katika kikosi cha PSG. Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amebainisha kuwa hali imebadilika. Mazungumzo ya mkataba mpya kati ya mchezaji huyo na klabu yake yamesimama, jambo ambalo linafungua mlango wa yeye kuondoka.
“Ukweli ni kwamba Barcola si ‘untouchable’ tena. Kuna uwezekano mkubwa wa yeye kuondoka Paris katika dirisha hili. Liverpool wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu sana tangu dirisha la 2025, na bado wanavutiwa na huduma yake,” alisema Romano.
Gharama kubwa kwa ‘The Reds’
Hata hivyo, usajili huu hautakuwa rahisi wala wa bei nafuu. Ripoti zinaeleza kuwa PSG huenda ikadai kiasi cha Euro milioni 150 (takriban Pauni milioni 128) ili kumwachia nyota huyo wa miaka 23. Ikiwa Liverpool itakubali kulipa ada hiyo, itakuwa ndiyo ada kubwa zaidi kuwahi kulipwa katika historia ya klabu hiyo, ikivunja rekodi waliyoweka kwa Alexander Isak msimu uliopita.
Kukosa Diomande ni heri?
Awali, Liverpool ilikuwa ikimnyatia Yan Diomande wa RB Leipzig, lakini dili hilo limeonekana kusuasua kutokana na mchezaji huyo kuvutiwa zaidi na PSG. Kiungo wa zamani wa Liverpool, Danny Murphy, anaamini kuwa kushindwa kumpata Diomande huenda kusiwe jambo mbaya kwa klabu hiyo.
Murphy alisema: “Kwa namna fulani, inaweza kuwa baraka. Barcola ni mchezaji ambaye tumeshuhudia akionyesha uwezo wake katika Ligi ya Mabingwa kwa misimu ya hivi karibuni, hivyo ni hatari ndogo ukilinganisha na kusajili mchezaji kwa pesa nyingi kwa msingi wa ahadi tu.”
Liverpool sasa inatarajiwa kupima uwezekano wa kukamilisha dili hili huku ikijua kuwa ushindani upo, kwani hata Arsenal imekuwa ikitajwa kufuatilia hali ya winga huyo ingawa si chaguo lao la kwanza.