Liverpool wafikia muafaka kumsajili Bradley Barcola kutoka PSG
Hatua kubwa ya Liverpool sokoni
Klabu ya Liverpool imepiga hatua muhimu katika jitihada zao za kuimarisha kikosi kufuatia kufikia makubaliano ya awali (agreement in principle) na Paris Saint-Germain kwa ajili ya kumsajili winga machachari, Bradley Barcola. Uhamisho huu unakuja baada ya Liverpool kukosa fursa ya kuwapata wachezaji wengine waliokuwa wakiwawinda awali, akiwemo Michael Olise.
Taarifa zinaeleza kuwa Barcola mwenyewe ameonyesha nia ya wazi ya kujiunga na Liverpool, akisisitiza kuwa hataki kuongeza mkataba wake na mabingwa hao wa Ufaransa ambao unaisha mwaka 2028. Aidha, ripoti zinaashiria kuwa mchezaji huyo alikuwa akipendelea kutua Anfield kuliko kujiunga na Arsenal.
Ada ya uhamisho na makubaliano
Awali, mazungumzo kati ya pande hizi mbili yalikuwa magumu kutokana na tofauti ya dau, huku PSG wakitaka kiasi cha pauni milioni 145, wakati Liverpool wakipanga kutumia kiasi cha pauni milioni 100. Hata hivyo, inaonekana pande zote mbili zimekubaliana kukutana katikati.
Ada ya uhamisho inatajwa kuwa ni karibu Euro milioni 128 (takriban pauni milioni 110), ikijumuisha nyongeza (add-ons) ambazo zinaonekana kuwa na uhalisia zaidi kufikiwa. Ingawa makubaliano yamefikiwa kikanuni, bado hakuna mkataba wowote uliotiwa saini rasmi hadi hivi sasa.
Maoni ya Emile Heskey
Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, Emile Heskey, ameunga mkono hatua ya klabu hiyo kumsajili Barcola, akiamini kuwa mchezaji huyo anaendana vizuri na falsafa ya soka la Liverpool.
“Kwa namna Liverpool wanavyocheza, na mtindo wa kiufundi aliozoea, Barcola anafaa kikamilifu. Ana kasi ya moja kwa moja na nguvu ambazo Liverpool wamekuwa wakizikosa tangu Luis Diaz alipoondoka. Anatoa tishio la kweli la ushambuliaji pembeni,” alisema Heskey.
Kuhusu maeneo mengine yanayohitaji kuimarishwa, Heskey aliongeza kuwa klabu hiyo bado inahitaji beki wa kati baada ya kuondoka kwa Ibrahima Konate, sambamba na kiungo wa kati atakayeweza kutoa ushindani kwa Alexis Mac Allister, huku akimpendekeza Adam Wharton wa Crystal Palace kama chaguo la kufikiriwa.