Liverpool yaikaribia saini ya Bradley Barcola huku PSG wakitafuta mbadala
Liverpool kwenye mchakato wa kumsaka mbadala wa Salah
Liverpool inaonekana kupata mwanga katika harakati zao za kusaka winga mahiri ambaye ataziba nafasi iliyoachwa na gwiji Mohamed Salah, ambaye aliondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu uliopita kutafuta changamoto mpya.
Katika harakati hizo, nyota wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, ndiye anayeonekana kuwa kipaumbele cha sasa cha kocha na uongozi wa Liverpool. Habari njema kwa mashabiki wa klabu hiyo ni kwamba mchezaji huyo hana nia ya kuongeza mkataba wake jijini Paris na ameonyesha wazi nia ya kutaka kujiunga na Liverpool.
PSG wajipanga na Mika Godts
Ili kufanikisha dili hili, kuna ishara kuwa mambo yanaanza kukaa sawa kwani PSG wameanza mchakato wa kusaka mbadala wa Barcola. Ripoti za mwandishi mahiri wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, zinaeleza kuwa mabingwa hao wa Ufaransa wameanza mazungumzo na Ajax kwa ajili ya kumsajili winga Mika Godts.
“Luis Campos amekutana na mchezaji huyo ana kwa ana nchini Ureno na Mika Godts amevutiwa sana na mradi wa Paris Saint-Germain. Yupo tayari kujiunga na timu hiyo, na makubaliano binafsi hayana shida,” alieleza Romano.
Ajax wanaripotiwa kuhitaji kiasi cha Euro milioni 60 ili kumwachia nyota huyo, na mazungumzo kati ya klabu hizo mbili yanaendelea huku PSG wakijaribu kuushusha bei hiyo.
Liverpool hawapo tayari kuvunja benki
Licha ya nia ya dhati ya kumnasa Barcola, Romano ameweka wazi kuwa Liverpool haiko tayari kufanya matumizi ya kijinga. Ingawa mazungumzo yanaendelea kati ya Liverpool, PSG, na mawakala wa mchezaji, klabu hiyo ya Anfield inahitaji kupata bei inayoeleweka.
“Liverpool haitalipa Euro milioni 170. Wanahitaji kupata bei ya kuridhisha. Mazungumzo yataendelea, na nawaambia mashabiki wa Liverpool watulie, hakutakuwa na maamuzi makubwa wikiendi hii, lakini kuanzia wiki ijayo tutaona mwelekeo wa mazungumzo hayo,” aliongeza Romano.
Kwa sasa, Liverpool wanaendelea kufanya kazi kwa uvumilivu huku wakihakikisha kuwa wanapata mchezaji mwenye viwango vya juu vya kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kabla ya dirisha la usajili kufungwa.