Skip to content

Liverpool yamtabulisha Bradley Barcola kwa staili ya kipekee ya 'BB29'

SokaNews
Updated: Published: Jumatano, 2 Septemba 2026 · 2 min read
liverpool bradleybarcola usajili adidas premierleague
Liverpool yamtabulisha Bradley Barcola kwa staili ya kipekee ya 'BB29'

Ujio mpya wa Barcola Anfield

Liverpool imethibitisha rasmi namba ya jezi atakayovaa winga mpya raia wa Ufaransa, Bradley Barcola, baada ya kukamilisha uhamisho wake wa rekodi kutoka Paris Saint-Germain (PSG) kwa ada ya pauni milioni 123. Mchezaji huyo atavaa jezi namba 29 mgongoni.

Katika kuanza maisha yake mapya ndani ya kikosi cha ‘The Reds’, klabu hiyo imetumia mbinu ya kipekee ya kimasoko kumtambulisha nyota huyo. Barcola atakuwa akitumia jina la ‘B.Barcola’ nyuma ya jezi yake, huku klabu ikimbandika jina la utani la ‘BB29’ katika machapisho mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii.

Mbinu inayowakumbusha vigogo

Staili hii ya kutumia herufi za jina na namba ya jezi (BB29) inatajwa kuwa ni mbinu ambayo imekuwa ikitumiwa na mastaa wakubwa duniani. Jina la utani la aina hii lilipata umaarufu mkubwa kupitia kwa Cristiano Ronaldo na alama yake ya ‘CR7’, ambayo ilitumika kumtofautisha na gwiji wa Brazil, Ronaldo Nazario, aliyefahamika kama ‘R9’.

Kampuni ya Adidas, ambayo ndiyo mdhamini wa jezi za Liverpool, inaonekana kutumia mbinu hiyo hiyo kwa mastaa wengine kama Lionel Messi kupitia mkusanyiko wa ‘LM10’. Sasa, wameamua kutumia mbinu hiyo hiyo kwa Barcola ili kumjenga kama nembo mpya ya kibiashara ndani ya klabu hiyo, hususan baada ya kuondoka kwa Mohamed Salah katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Ofa maalum kwa mashabiki

Ili kuongeza hamasa ya mauzo ya jezi mpya, Liverpool imetangaza kutoa huduma ya bure ya kuchapa majina na namba kwenye jezi kwa siku chache zijazo. Hatua hii inaenda sambamba na uzinduzi wa jezi ya tatu ya timu hiyo kwa msimu wa 2026/27, inayokamilisha muonekano wa mavazi ya Adidas kwa msimu huu.

Ushirikiano na Adidas unavyolipa

Uhusiano wa kibiashara kati ya Liverpool na Adidas ni miongoni mwa mikataba mikubwa zaidi katika soka, ambapo kampuni hiyo hulipa hadi pauni milioni 60 kwa mwaka ili kusambaza vifaa vya klabu hiyo. Mbali na jezi za kuchezea, ushirikiano huu umeleta bidhaa mbalimbali ikiwemo viatu maalum vya Liverpool na nguo za ‘retro’.

Hivi karibuni, klabu imezindua pia mkusanyiko mpya wa ‘Adidas Teamgeist’, ambao umebeba mguso wa kihistoria wa jezi zilizotumiwa na klabu hiyo katikati ya miaka ya 2000, zikiwa na mchanganyiko wa rangi ya kijani na nyeupe. Mashabiki wa Liverpool wanatarajiwa kupokea ujio wa Barcola kwa matumaini makubwa huku wakisubiri kuona kama ataziba vyema pengo la mastaa walioondoka.