Liverpool yaweka mezani kitita cha Pauni milioni 56 kumnasa Endrick
Liverpool yajipanga upya baada ya kuondoka kwa Salah
Klabu ya Liverpool inaonekana kuingia kwenye kasi mpya ya usajili katika dirisha hili, huku ikionyesha nia ya dhati ya kuziba pengo lililoachwa na gwiji Mohamed Salah, ambaye kwa sasa anakipiga nchini Uturuki katika klabu ya Trabzonspor.
Baada ya kufanikiwa kumsajili Victor Munoz kutoka Osasuna, beki Ronald Araujo kwa mkopo kutoka Barcelona, na kukamilisha usajili wa Jeremy Jacquet kutoka Rennes, sasa macho ya majogoo hao wa Anfield yameelekezwa kwa washambuliaji wawili matata: Bradley Barcola na nyota wa Real Madrid, Endrick.
Barcola ndiye kipaumbele cha sasa
Taarifa za uhakika kutoka kwa mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, zinaeleza kuwa Liverpool wapo katika hatua za mwisho za mazungumzo kumnasa Bradley Barcola kutoka Paris Saint-Germain (PSG).
Romano amedokeza kuwa PSG wapo tayari kuachana na winga huyo mwenye kasi, kwani wamejaa washambuliaji wengi wenye majina makubwa kama vile Desire Doue, Ousmane Dembele, na Khvicha Kvaratskhelia.
Liverpool wanajadili dili la Barcola. Wana imani kubwa na wanaendelea kushinikiza ili kukamilisha usajili huu. Tunatarajia dili hili kuharakishwa kuanzia wiki hii, kwani tayari kuna makubaliano ya awali kati ya Liverpool na mchezaji mwenyewe kuhusu maslahi binafsi.
Ofa ya Pauni milioni 56 mezani kwa Endrick
Si Barcola pekee anayewindwa, kwani ripoti kutoka nchini Hispania zinasema Liverpool wamepiga hodi rasmi Real Madrid kwa ajili ya mshambuliaji kijana, Endrick. Inadaiwa kuwa Liverpool wameweka mezani ofa ya Euro milioni 65, ambayo ni sawa na takriban Pauni milioni 56.
Endrick, ambaye msimu uliopita alikuwa kwa mkopo Lyon, anaonekana kupata wakati mgumu kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid kufuatia kuingia kwa nyota kama Yan Diomande. Hali hiyo inawapa Liverpool matumaini kuwa klabu hiyo ya jijini Madrid inaweza kuwa tayari kumuuza kijana huyo ili kufidia gharama walizotumia kumsajili kutoka Palmeiras mwaka 2024.
Inaelezwa kuwa mara tu Liverpool itakapokamilisha dili la Bradley Barcola, itajikita kikamilifu kuhakikisha saini ya Endrick inapatikana. Kocha wa Madrid, Jose Mourinho, ndiye atakayetoa uamuzi wa mwisho kama nyota huyo ataondoka au atabaki kuendeleza kipaji chake Bernabeu. Mashabiki wa Anfield sasa wanavuta subira kuona kama maboresho haya yatawapa nguvu mpya ya kupambana katika michuano ijayo.