Skip to content

Fabrizio Romano: Liverpool bado wapo kwenye mbio za kumsajili Bradley Barcola

SokaNews
Updated: Published: Jumamosi, 15 Agosti 2026 · 2 min read
liverpool bradleybarcola psg usajili fabrizioromano premierleague
Fabrizio Romano: Liverpool bado wapo kwenye mbio za kumsajili Bradley Barcola

Liverpool haijakata tamaa kwa Barcola

Wakati gumzo la usajili likiendelea barani Ulaya, mtaalamu wa masuala ya uhamisho wa wachezaji, Fabrizio Romano, ametoa ufafanuzi kuhusu hatima ya winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, na kuhusishwa kwake na klabu ya Liverpool.

Licha ya kuwepo kwa ripoti za hivi karibuni zilizodai kuwa Liverpool huenda ikasitisha mazungumzo na PSG, Romano amesisitiza kuwa taarifa hizo si sahihi. Kwa mujibu wa mwandishi huyo, klabu hiyo ya Anfield bado ina nia ya dhati ya kumsajili nyota huyo ambaye anatazamwa kama mrithi sahihi wa Mohamed Salah.

Hali ya mazungumzo ikoje?

Romano amesema kuwa klabu hizo mbili zinaendelea kuwasiliana, ingawa kuna changamoto ya kifikia muafaka kuhusu ada ya uhamisho. PSG inaripotiwa kuhitaji kiasi cha pauni milioni 145 ili kumwachia winga huyo, kiasi ambacho kinaonekana kuwa kikubwa ikilinganishwa na ofa ya Liverpool.

“Liverpool wanazungumza kuhusu Barcola. Nimekuwa nikiamini taarifa hizi tangu mwezi Aprili na Mei, wakati ambapo watu wengi walikuwa wakisema Barcola hawezi kuondoka PSG. Ninaendelea kusimamia msimamo wangu; Liverpool bado wanajaribu kumsajili. Bado kuna pengo la kifedha kati ya kile PSG inachotaka na ofa ya Liverpool, lakini mazungumzo yanaendelea. Makubaliano na mchezaji binafsi yapo tayari, na biashara bado ipo hai,” alisema Romano.

Changamoto kwenye eneo la kiungo

Wakati shughuli za usajili zikiendelea, nguli wa klabu ya Liverpool, Jamie Carragher, ametoa angalizo kuhusu muundo wa kikosi hicho kuelekea msimu mpya. Kwa mtazamo wake, eneo la kiungo bado linaonekana kuwa na matatizo yaleyale yaliyoiandama timu hiyo msimu uliopita.

Carragher anaeleza kuwa bado kuna nafasi wazi katikati ya uwanja ambayo wapinzani wanaitumia kuleta madhara. Aliongeza kuwa matumizi ya Dominik Szoboszlai kama kiungo wa kati badala ya jukumu lake la asili la namba 10, yanaweza kuongeza changamoto hiyo kwani mfumo unaotumika sasa unawaacha viungo wakiwa na majukumu makubwa ya kukimbia uwanja mzima (box-to-box).

Liverpool imefanikiwa kumsajili Ronald Araujo, Jeremy Jacquet, na Victor Munoz, lakini inaonekana bado inahitaji nguvu mpya kwenye safu ya ushambuliaji ili kuziba pengo la Salah na kuimarisha kikosi kinachotaka kushindana kwenye mataji makubwa.