Louis Saha: Ayden Heaven ni lulu ya Man Utd, kushindwa kumsajili Kane ilikuwa makosa
Saha amvulia kofia Ayden Heaven
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Louis Saha, ametoa maoni yake kuhusiana na mustakabali wa kikosi cha sasa cha ‘Mashetani Wekundu’, akisisitiza kuwa klabu hiyo ina hazina kubwa katika beki kijana Ayden Heaven. Heaven, ambaye alijiunga na United akitokea Arsenal mwezi Februari 2025, amekuwa akionyesha kiwango kikubwa kinachomvutia Saha.
Saha anaamini kuwa Heaven ni mchezaji mwenye uwezo wa kipekee, hasa kutokana na umakini wake uwanjani. Alisema:
“Kila ninapomuona akicheza, naona mchezaji asiyekuwa na makosa mengi hata akiwa kijana mdogo, na hiyo ni sifa adimu kwa mabeki. Ni ngumu zaidi kucheza kwa kiwango hicho katika kikosi cha sasa cha Manchester United ikilinganishwa na enzi zetu.”
Changamoto ya wachezaji vijana sasa
Katika uchambuzi wake, Saha alilinganisha mazingira ya sasa na yale aliyokutana nayo wakati akicheza Old Trafford. Kwa mujibu wa Saha, ilikuwa rahisi kwa wachezaji vijana kufanikiwa nyakati hizo kwa sababu ya kuwepo kwa magwiji kama Rio Ferdinand, Roy Keane, na Michael Carrick waliokuwa tayari kuwafundisha.
Saha anaamini kuwa wachezaji kama Heaven na Leny Yoro wanahitaji kuungwa mkono na uongozi wa INEOS pamoja na benchi la ufundi linaloongozwa na Michael Carrick ili waweze kukomaa kupitia mechi za mashindano makubwa kama Champions League na FA Cup.
”Kushindwa kumsajili Kane ilikuwa wazimu”
Saha hakuishia hapo, pia alizungumzia uamuzi wa Manchester United kushindwa kumsajili Harry Kane kabla ya mshambuliaji huyo kutimkia Bayern Munich mwaka 2023. Kwake, huo ulikuwa uamuzi mbaya uliokigharimu klabu hiyo mataji mengi.
“Manchester United wangekuwa wamebeba mataji mengi zaidi kama wangesajili Harry Kane miaka miwili iliyopita. Ilikuwa ni uamuzi wa kishabiki na wa kipuuzi (insane decision) kutomleta hapa. Don’t tell me (Usinidanganye) kuwa United isingekuwa bingwa wa Premier League au hata Champions League kama angekuwa nao,” alisisitiza Saha.
Saha aliongeza kuwa idadi ya mabao na pasi za mwisho alizonazo Kane ni ushahidi tosha wa ubora wake, akiamini kuwa pesa yoyote iliyohitajika kumsajili ingekuwa na thamani kubwa kuliko hali ya sasa.