Manchester City hatiani kwa mashtaka 114 ya FFP: Vilabu vya EPL vyapanga kudai fidia
Tetemeko la ardhi Etihad: Manchester City pabaya
Soka la Uingereza liko katika hali ya sintofahamu kufuatia taarifa nzito kuwa Manchester City wamepatikana na hatia katika mashtaka 114 kati ya 115 yaliyokuwa yakiwakabili kuhusiana na ukiukaji wa kanuni za matumizi ya fedha (FFP). Hii inafuatia uchunguzi wa kina wa muda mrefu uliokuwa ukifanywa na kamati huru ya Premier League.
Kesi hii, ambayo ilianza tangu mwaka 2023 kufuatia tuhuma za mwenendo wa klabu hiyo kati ya mwaka 2009 na 2018, sasa imefika hatua ya maamuzi ambayo yanaweza kubadilisha historia ya soka nchini Uingereza milele.
Vilabu vya ‘Big Six’ vyataka fidia
Hali inazidi kuwa ngumu kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza, kwani si tu wanakabiliwa na adhabu kutoka kwa mamlaka, bali pia shinikizo kutoka kwa wapinzani wao wa moja kwa moja.
Taarifa zinaeleza kuwa vilabu vinne vikubwa nchini Uingereza—Manchester United, Arsenal, Liverpool, na Tottenham Hotspur—tayari vimeanza mikakati ya kisheria kutaka kulipwa fidia. Inakadiriwa kuwa vilabu hivi vinaweza kudai zaidi ya pauni milioni 200 kwa pamoja.
Akifafanua juu ya hali hiyo, mwandishi Miguel Delaney amesema:
“Idadi ya wapinzani wanapanga kufuata michakato ya kisheria, huku kukiwa na matarajio kwamba City watapatikana na hatia katika karibu mashtaka yote… Angalau vilabu vinne vimehifadhi haki zao za kudai fidia kutokana na kupoteza mapato chini ya Kifungu cha W cha kanuni za mashindano.”
Nini kinafuata kwa City?
Kampuni za kisheria zinazowakilisha vilabu hivyo zimekuwa zikifanya mawasiliano ya kina ili kuhakikisha haki za wateja wao zinalindwa kabla ya muda wa kisheria wa kushtaki kumalizika. Hatua hii inaongeza presha kwa Manchester City ambao wamekuwa wakisisitiza kutokuwa na hatia yao tangu kesi hii ilipoanza.
Klabu hiyo sasa inakabiliwa na uwezekano wa kupewa adhabu kali ambazo zinaweza kujumuisha:
- Faini kubwa ya kifedha.
- Kupokonywa pointi kwenye msimamo wa ligi.
- Kupigwa marufuku ya kufanya usajili.
- Kuvuliwa mataji ya Premier League waliyoshinda.
- Kufukuzwa kabisa kwenye ligi.
Ingawa Manchester City bado wana nafasi ya kukata rufaa, uamuzi huu wa kamati huru ni pigo kubwa kwa taswira ya klabu hiyo. Mashabiki na wadau wa soka duniani sasa wanaelekeza macho yao kusubiri hatua inayofuata katika sakata hili ambalo limepewa jina la ‘sakata la karne’ katika soka la Uingereza.