Skip to content

Manchester City wamthibitisha Enzo Maresca, Chelsea watoa tamko zito

SokaNews
Updated: Published: Jumatatu, 29 Juni 2026 · 2 min read
manchestercity chelsea enzomaresca premierleague usajili kocha
Manchester City wamthibitisha Enzo Maresca, Chelsea watoa tamko zito

Hatima ya Enzo Maresca hatimaye imejulikana

Manchester City wamehitimisha utata wa muda mrefu baada ya kumtangaza rasmi Enzo Maresca kuwa kocha wao mkuu. Maresca amesaini mkataba wa miaka mitatu katika klabu hiyo ya Etihad, akichukua mikoba iliyoachwa na Pep Guardiola.

Ujio wa Maresca ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu, lakini mchakato huo ulichelewa kutokana na mazungumzo marefu ya kifuta jasho (compensation) kati ya Manchester City na Chelsea, klabu ambayo kocha huyo alikuwa akiifundisha kabla ya kuondoka ghafla mwanzoni mwa mwaka 2026.

Chelsea watoa dukuduku lao

Baada ya taarifa hiyo kutoka, Chelsea waliamua kuweka wazi hisia zao kupitia taarifa ndefu na nzito iliyochapishwa kwenye tovuti yao. Klabu hiyo imeeleza jinsi walivyohisi kusalitiwa na uamuzi wa kocha huyo.

“Tulihisi kuumizwa kwa sababu tuliamini kuwa akili na moyo wake vilikuwa kwenye klabu nyingine na fursa nyingine, licha ya kuwa alikuwa amewasili Chelsea mwaka mmoja uliopita,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Chelsea.

Chelsea walifafanua kuwa katika kipindi cha vuli mwaka jana, walipata taarifa kuwa Maresca alikuwa na nia ya kurithi mikoba ya Guardiola. Licha ya kuwa na mkataba wa muda mrefu, kocha huyo alichukua uamuzi wa kujiuzulu ghafla mwezi Desemba 2025, hatua ambayo klabu hiyo ilisema iliwalazimu kukubali ili kulinda heshima ya timu.

Makubaliano ya kifedha

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Chelsea wamefanikiwa kupata kitita cha pauni milioni 17 kama fidia kutoka kwa Manchester City. Aidha, klabu hiyo imethibitisha kuwa wamefikia makubaliano ya siri na kocha huyo ambapo naye atalazimika kulipa fidia.

Kuhusu mustakabali wao, Chelsea wameweka imani yao kwa kocha Xabi Alonso, wakimsifu kama mtu mwenye uelewa mkubwa wa soka na mtaalamu mwenye maadili ya hali ya juu anayeweza kuleta mafanikio wanayoyahitaji mashabiki.

Ujumbe wa Maresca

Kwa upande wake, Enzo Maresca amekiri kosa lake na kuomba radhi kwa vurugu zilizotokea ndani ya Chelsea kutokana na uamuzi wake wa kuondoka katikati ya msimu.

“Uamuzi ulikuwa wangu pekee. Kujiuzulu kwangu Chelsea kulifungua njia ya mimi kujiunga na Manchester City, klabu ambayo naifahamu vyema. Natambua kuwa kuondoka kwangu katikati ya msimu kulisababisha usumbufu mkubwa kwa klabu na ninaomba radhi kwa hilo,” alisema Maresca.