Manchester City yajipanga kulipa £120m kumnasa Enzo Fernandez kutoka Chelsea
Man City yafukuzia saini ya Enzo Fernandez
Klabu ya Manchester City inaonekana kuongeza kasi katika harakati za kutafuta mrithi wa Rodri, huku ripoti mpya zikionyesha kuwa mabingwa hao wa England wako tayari kukidhi dau la pauni milioni 120 (takriban shilingi bilioni 400 za Kitanzania) linalohitajika na Chelsea ili kumuachia kiungo wao, Enzo Fernandez.
Baada ya kuondoka kwa Rodri kuelekea Barcelona kwa ada inayofikia pauni milioni 65, Manchester City imejikuta ikihitaji marekebisho ya haraka katika safu yao ya kiungo. Licha ya mipango yao ya kumsajili staa wa Lille, Ayyoub Bouaddi, kocha Enzo Maresca anaonekana kumpa kipaumbele Fernandez ili kuimarisha eneo la kati la uwanja.
Chelsea wadhibiti hali
Ingawa kulikuwa na makubaliano ya awali yaliyowekewa ukomo wa muda na Chelsea, ambayo yalipitwa na wakati Ijumaa iliyopita, mwandishi nguli wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amebainisha kuwa Manchester City haijakata tamaa.
“Manchester City bado inamfikiria Enzo Fernandez. Hawajakata tamaa hata baada ya muda wa mwisho kupita. Sasa hivi ni Chelsea ndiyo inayoamua na kutathmini hali ilivyo. City bado wanawasiliana na wakala wa mchezaji,” alisema Romano kupitia chaneli yake ya YouTube.
Mabadiliko ya kikosi Man City
Kwa mujibu wa mwandishi Pete O’Rourke, Manchester City iko kwenye mchakato wa kuijenga upya safu yake ya kiungo baada ya kuondokewa na nyota kadhaa wakiwemo Bernardo Silva, Rodri, na Tijjani Reijnders aliyejiunga na Ligi ya Saudi Arabia. Pesa zilizopatikana kutokana na mauzo hayo zinatajwa kuwa msingi mkuu wa City kuwa na uwezo wa kifedha wa kumsajili Fernandez.
Chelsea yajipanga kutoa washambuliaji watatu
Katika upande mwingine, Chelsea ina mpango wake wa kiuchumi ili kuongeza bajeti ya usajili. Ripoti zinasema kuwa klabu hiyo inalenga kukusanya kiasi cha pauni milioni 140 kwa kuuza washambuliaji watatu. Wachezaji wanaotajwa kuwekwa sokoni ni Nicolas Jackson (pauni milioni 65), Liam Delap (pauni milioni 50), na Marc Guiu (pauni milioni 25).
Hali hii inafanya dirisha hili la usajili kuwa la kuvutia, huku macho ya mashabiki yakiwa kwa viongozi wa Man City na Chelsea kuona kama makubaliano haya yatafikiwa kabla ya dirisha kufungwa rasmi.