Dili la Mateus Fernandes: Liverpool Kuingilia Kati Vita ya Man Utd na West Ham
Manchester United wanaendelea na mchakato wa kusaka saini ya kiungo wa West Ham United, Mateus Fernandes, lakini kikwazo kikubwa kimeibuka huku mahasimu wao wa jadi, Liverpool, wakipiga hodi kutaka kuvuruga dili hilo.
Mashetani Wekundu tayari wamekamilisha usajili wa nyota wa Atalanta, Ederson, msimu huu wa kiangazi na kuna taarifa kuwa alifanyiwa vipimo vya afya wiki iliyopita huko New York.
Hata hivyo, mabadiliko makubwa yanatarajiwa katika safu ya viungo ya United. Klabu hiyo inapanga kumuuza Manuel Ugarte, huku Casemiro akiwa ameshaondoka bure, jambo linalofanya miamba hiyo ya Old Trafford kuhitaji viungo wengine wawili wapya.
West Ham Weka Ngumu Kwenye Dau la Fernandes
Ingawa lengo lao kuu lilikuwa ni Elliot Anderson wa Nottingham Forest, sasa inaonekana kiungo huyo wa kimataifa wa England atajiunga na Manchester City, ambao wako tayari kutoa dau kubwa. Hali hiyo imefanya United kuelekeza nguvu zao kwa Mateus Fernandes wa West Ham, na kuna tetesi kuwa tayari wamekubaliana masuala binafsi na mchezaji huyo.
Taarifa kutoka mtandao wa The Athletic zinasema kuwa masuala binafsi hayatakuwa shida, lakini dau kubwa la pauni milioni 80 linalodaiwa na West Ham ndilo linaloweza kukwamisha uhamisho huo.
Ripoti hiyo inaeleza:
“Manchester United wanaendelea kufuatilia uwezekano wa kumsajili Mateus Fernandes kutoka West Ham United. Masuala binafsi kati ya United na Fernandes hayatarajiwi kuwa kikwazo. Lakini hata kama Old Trafford ndio chaguo la mchezaji, ushindani wa kuwania saini yake unaweza kupandisha na kuimarisha bei yake.”
“Mahitaji ya West Ham ya pauni milioni 80 yanatarajiwa kuwa kikwazo kikubwa. United wameonyesha kusita kulipa kiasi hicho, lakini ikiwa mpinzani wao atakuwa tayari kukaribia dau hilo la West Ham, uongozi wa Old Trafford utalazimika kufanya maamuzi magumu.”
United bado hawajawasilisha ofa rasmi kwa Fernandes, ingawa inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Liverpool Wajiandaa Kupindua Meza
Habari hizi zimekuja siku moja baada ya ripoti kudai kuwa Liverpool wamejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuvuruga dili hilo la United kwani nao wanatafuta kiungo mwenye nguvu na kasi ili kuimarisha kikosi chao.
Inaarifiwa kuwa Liverpool walifanya mawasiliano na West Ham wiki mbili zilizopita ili kufahamu mazingira na kiasi kinachohitajika kumnunua kiungo huyo wa kimataifa wa Ureno, ambaye alifunga mabao matatu na kutoa pasi nne za mabao katika michezo 36 ya Ligi Kuu ya Uingereza msimu wa 2025-26.
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amethibitisha kuwa Liverpool wamekuwa wakipiga simu kuulizia kuhusu Fernandes wakati wakitathmini machaguo yao ya viungo.
Romano alisema:
“Nitawaambia kitu ambacho hakikuwa wazi sana siku na wiki za hivi karibuni. Liverpool walipiga simu wiki mbili zilizopita kufahamu hali ya Fernandes pale West Ham, kujua bei na masharti yake, lakini hawakurudi na ofa yoyote au mazungumzo rasmi. Lakini walipiga simu, hilo nina uhakika nalo. Tottenham na Man United nao wapo bize na dili hili, kwa hiyo kuna klabu nyingi zinazohusika. Mchezaji huyu atakuwa ghali sana, zaidi ya pauni milioni 85. Hii inamaanisha Liverpool wanafanyia kazi usajili wa viungo.”