Fabrizio Romano aondoa utata wa Man Utd kumsajili Francisco Conceicao
Man Utd hawana mpango na Conceicao
Mchambuzi maarufu wa masuala ya usajili barani Ulaya, Fabrizio Romano, ameweka nukta mwisho wa tetesi zilizokuwa zikidai kuwa Manchester United inafanya jitihada za kumsajili winga wa Juventus, Francisco Conceicao.
Katika siku za hivi karibuni, vyombo mbalimbali vya habari, hususan kutoka Italia, viliripoti kuwa klabu hiyo ya Old Trafford inamfukuzia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, huku kukiwa na madai kuwa kocha Michael Carrick anamwona kama mchezaji anayefaa kabisa kwa falsafa yake. Hata hivyo, Romano amekanusha vikali taarifa hizo.
Hakuna mawasiliano yoyote
Akizungumza kupitia chaneli yake ya YouTube, Romano alisisitiza kuwa hakuna ukweli wowote kuhusu mpango huo, akibainisha kuwa hajapata taarifa yoyote ya kuaminika inayohusisha pande hizo mbili.
“Guys, sina uthibitisho wowote wa hilo, hata simu moja haijapigwa. Sio kwamba Conceicao sio mchezaji wa kiwango cha Manchester United, la hasha, lakini ni kwa sababu Manchester United wanaonekana kuwa na utulivu katika nafasi hiyo kuliko sehemu nyingine yoyote ya kikosi chao,” alisema Romano.
Romano aliongeza kuwa United tayari ina wachezaji wazuri katika nafasi ya winga kama vile Bryan Mbeumo na Amad Diallo, ambao wamekuwa wakionyesha kiwango bora, jambo linalofanya hitaji la kumsajili winga mwingine kuwa si la msingi kwa sasa.
Juventus hawana haraka ya kuuza
Sio tu Manchester United waliojitokeza kukanusha taarifa hizo, bali hata upande wa Juventus hauna mpango wa kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Ureno. Kulingana na mchambuzi huyo, kwa sasa hakuna mazungumzo yoyote kati ya pande zote zinazohusika.
“Kufikia leo, Juventus hawajaribu kikamilifu kumuuza Conceicao, wala Conceicao hajaribu kuondoka Juve. Ni hali inayofanana kidogo na ile ya Bremer mwezi Juni, ambapo kila mtu alisema Bayern walikuwa wanamtaka, lakini haikuwahi kutokea,” aliongeza Romano.
Ingawa Romano hakufunga mlango kabisa kwa siku za usoni ikiwa ofa nono itatolewa na klabu yoyote, alisisitiza kuwa kwa sasa tetesi za kuhamia Manchester United ni habari ambazo hazina msingi wowote. Hivyo, mashabiki wa ‘Mashetani Wekundu’ wanapaswa kuzipuuza taarifa hizo na kuzingatia kile kinachoendelea uwanjani chini ya kocha Michael Carrick.