Manchester United kukubali kupoteza kipaji matata JJ Gabriel
United yajipanga kwa maisha bila Gabriel
Klabu ya Manchester United inaonekana kufikia ukingoni mwa uvumilivu wake katika harakati za kumbakiza mmoja wa vipaji bora zaidi vya akademi yao, JJ Gabriel. Taarifa kutoka ndani ya Old Trafford zinaeleza kuwa viongozi wa klabu hiyo wameanza kukubali uhalisia kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 15 huenda akaondoka hivi karibuni.
Gabriel, ambaye amekuwa gumzo kutokana na kiwango chake bora ikiwemo kufunga hat-trick ndani ya kipindi kimoja katika mchezo wake wa kwanza wa UEFA Youth League dhidi ya FC Sabah, anatajwa kuwa na ndoto ya kucheza soka nchini Hispania. Vilabu vikubwa vya Barcelona na Real Madrid vimekuwa vikitajwa kama sehemu inayomvutia zaidi nyota huyu chipukizi.
Utafutaji wa mbadala umeanza
Kufuatia hali hiyo, Manchester United haijakaa kizembe. Idara ya usajili ya klabu hiyo imeshaanza kusaka mrithi wake barani Ulaya. Jina linalotajwa kwa sasa ni kiungo mshambuliaji wa RC Lens, Mezian Mesloub, ambaye ni raia wa Ureno na anayechezea timu ya taifa ya Ureno chini ya umri wa miaka 17.
Mesloub tayari ameshaanza kupata uzoefu wa kucheza soka la ushindani, ikiwemo kucheza timu ya wakubwa ya Lens na hata kwenye michuano ya Champions League. Skauti wa United wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu sana kijana huyu ili kuona kama anaweza kuwa mbadala sahihi wa Gabriel.
Maoni ya Wayne Rooney
Legend wa Manchester United, Wayne Rooney, ambaye amekuwa akimfahamu Gabriel kwa muda mrefu kupitia akademi, anaamini kuwa kuondoka kwa kijana huyo hakuja kwa ghafla. Akizungumza kwenye Stick to United, Rooney alisema:
“Nimeona JJ akikua, amekuwa kwenye timu ya mtoto wangu Kai kwa miaka mingi na nadhani yeyote aliyekuwa karibu na hali hii alijua jambo hili linakuja. Manchester United wamefanya kila waliloweza, wamefanya kila kitu kumfanya abaki klabuni.”
Rooney aliongeza kuwa Gabriel amekuwa akipata huduma ya kipekee klabuni hapo kama mchezaji mwenye kipaji cha aina yake, lakini hamu yake ya kutaka kucheza Hispania imekuwapo tangu akiwa na umri wa miaka 12 au 13.
Ujumbe kwa wachezaji wengine
Rooney amesisitiza kuwa klabu haipaswi kulazimisha kubaki kwa mchezaji ambaye hana nia ya kuwepo hapo. Aliongeza:
“Kama kijana hupendi kuwa klabuni, sidhani kama unapaswa kubaki. Nadhani hilo linatuma ujumbe mbaya kwa wachezaji wengine klabuni ambao wao wanatamani sana kuwepo hapo.”
Kwa sasa, mashabiki wa United wanabaki kusubiri kuona hatma ya kijana huyo, huku klabu ikijipanga kuanza ukurasa mpya wa kukuza vipaji vingine kama Mezian Mesloub.