Skip to content

Manchester United yafanya mawasiliano kumnasa kiungo wa Tottenham, Lucas Bergvall

SokaNews
Updated: Published: Jumanne, 28 Julai 2026 · 2 min read
manchesterunited tottenham lucasbergvall usajili premierleague
Manchester United yafanya mawasiliano kumnasa kiungo wa Tottenham, Lucas Bergvall

United yataka kuimarisha kiungo

Manchester United inaendelea na pilikapilika za kusuka upya safu yake ya kiungo kuelekea msimu mpya wa 2026/27. Baada ya kufanikiwa kuwanasa Youri Tielemans kutoka Aston Villa na Andrey Santos kutoka Chelsea, klabu hiyo sasa inatafuta kiungo wa tatu ili kukamilisha maboresho hayo chini ya kocha Michael Carrick.

Awali, mipango ya United ilikuwa kumsajili Ederson kutoka Atalanta, lakini dili hilo lilikwama kutokana na matatizo yaliyojitokeza wakati wa vipimo vya afya. Sasa, taarifa mpya zinaonyesha kuwa miamba hiyo ya Old Trafford imegeukia uwezekano wa kumsajili Lucas Bergvall kutoka Tottenham Hotspur.

Bergvall anatarajiwa kuondoka Spurs

Kiungo huyo raia wa Sweden, Bergvall, anaonekana kutokuwa na nafasi ya uhakika kikosini Tottenham kutokana na ujio wa wachezaji wapya kama Sandro Tonali na Mateus Fernandes. Mwandishi Fabrizio Romano amebainisha kuwa mchezaji huyo anahitaji kuondoka ili kupata muda wa kucheza mara kwa mara.

“Lucas Bergvall anatarajiwa kuondoka Tottenham msimu huu. Amewaambia viongozi kuwa anahitaji kucheza mara kwa mara na yuko tayari kwa changamoto mpya. Hataki kutumia msimu mzima benchi au kucheza dakika kumi kila baada ya wiki mbili,” alisema Romano.

Mashindano makali ya usajili

Ukiachilia mbali Manchester United, klabu nyingine kama Nottingham Forest, Newcastle United, na Brighton nazo zimeonyesha nia ya kumsajili staa huyo. Ripoti zinaeleza kuwa Tottenham imeweka dau la kuanzia kati ya paundi milioni 50 hadi 60 ili kumwachia kiungo huyo.

Ingawa Nottingham Forest inatajwa kuweka ofa kubwa ya kifedha, Newcastle inajaribu kumshawishi mchezaji huyo kwa kumpa mradi wenye ushindani na malengo makubwa. Kwa upande wa Manchester United, mawasiliano yamekwisha anza, na sasa mashabiki wanataraji kuona kama klabu yao itaweza kufanikiwa katika ushindani huu mkali wa kumpata kiungo huyo chipukizi.