Fabrizio Romano afunguka kuhusu mpango wa Man Utd kumsajili Alejandro Balde
Man Utd yafukuzia saini ya Alejandro Balde
Klabu ya Manchester United inaendelea na mikakati yake ya kuimarisha safu ya ulinzi, safari hii ikimweka kwenye rada beki wa pembeni wa Barcelona, Alejandro Balde. Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, klabu hiyo ya Old Trafford bado inafanya mazungumzo na wakala maarufu Jorge Mendes ili kuona kama dili hilo linawezekana.
Baada ya kufanikiwa kukamilisha usajili wa viungo wake walioingia kwenye orodha ya kipaumbele, ambao ni Youri Tielemans, Andrey Santos, na Carlos Baleba, INEOS sasa wameelekeza nguvu zao katika kutafuta beki wa kushoto atakayeimarisha kikosi hicho. Kabla ya hapo, United walikuwa wakimfukuzia Lewis Hall kutoka Newcastle, lakini ugumu wa dau la usajili uliwalazimu kutafuta njia mbadala.
Msimamo wa Balde na Barcelona
Ingawa kumekuwa na taarifa za uwezekano wa United kumsajili Balde kwa mkopo, hali ya mambo bado si shwari kutokana na msimamo wa mchezaji mwenyewe. Romano amebainisha kuwa beki huyo wa kimataifa wa Hispania hana mpango wa kuondoka Camp Nou kwa siri, bali yupo tayari tu kuondoka endapo klabu yake ya Barcelona itaamua hivyo.
Akizungumza kupitia chaneli yake ya YouTube, Romano alisema:
“Kwa sasa, kama nilivyosema mara nyingi, Balde hasukumiwi kuondoka Barcelona. Ikiwa Barcelona watamwambia Balde kuwa wamekubaliana na klabu nyingine na inabidi aondoke, basi atafanya hivyo. Lakini yeye mwenyewe haonyeshi dalili za kutaka kuondoka. Anaikubali klabu na jiji la Barcelona, hivyo anafurahia kuwepo hapo.”
Changamoto za kifedha
Romano aliongeza kuwa Manchester United bado wanawasiliana na wakala wake, Jorge Mendes, lakini kuna vikwazo vya kifedha ambavyo vinatakiwa kutatuliwa ili dili hilo liweze kufanikiwa. Kwa sasa, hali ya mkataba na masharti ya usajili inaonekana kuwa na changamoto kwa upande wa United, kwani gharama zinazotajwa zinaonekana kuwa kubwa sana kwao.
“Manchester United bado wanawasiliana na Jorge Mendes kuhusu fursa hii, lakini kwa sasa masharti yote ya dili hili yanatakiwa kubadilika, vinginevyo gharama zinakuwa kubwa mno,” aliongeza Romano.
Kuelekea siku za mwisho za dirisha hili la usajili, mashabiki wa United wanasubiri kuona kama uongozi utafanikiwa kupunguza gharama hizo au kama wataelekeza nguvu zao kwa walengwa wengine kama David Raum wa RB Leipzig na Jorge Salinas wa Racing Santander ambao pia wamekuwa wakihusishwa na timu hiyo.