Manchester City yakabiliwa na shinikizo kubwa, wapinzani wataka adhabu kali zaidi ya kushushwa daraja
Hatima ya Manchester City kujulikana hivi karibuni
Manchester City ipo katika wakati mgumu baada ya jopo huru kuthibitisha kuwa klabu hiyo ina hatia katika mashtaka yote yanayohusu kukiuka kanuni za kifedha za Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League). Tuhuma hizo zinahusu kipindi cha miaka tisa, ambapo klabu hiyo ilidaiwa kupanga mikataba hewa na washirika wa kibiashara ili kuongeza mapato na kupunguza gharama kwa kiasi kinachozidi pauni milioni 900.
Kwa mujibu wa utaratibu mpya wa Ligi Kuu, maamuzi ya mwisho kuhusu adhabu dhidi ya City yanaweza kutoka mapema Januari mwaka ujao. Hii ni baada ya kuwepo kwa mchakato wa kukata rufaa ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya wiki 12, huku jopo likipewa siku 30 za kutoa hukumu baada ya hapo.
Wapinzani wataka adhabu kubwa
Wakati City ikitarajiwa kupambana na tuhuma hizi kwa kukata rufaa, shinikizo kutoka kwa klabu nyingine za Premier League limezidi kuongezeka. Wakuu wa klabu hizo wanaona kuwa adhabu ya kushushwa daraja pekee haitoshi kwa ukubwa wa kosa hilo.
Akizungumza na gazeti la The Guardian, chanzo kimoja kutoka katika moja ya klabu hizo kilisema:
“Kushushwa daraja kwenda Championship kwa msimu mmoja hakutoshi. Tume inapaswa kufikia adhabu ambayo ni sawia na ukubwa wa udanganyifu wa makusudi uliofanyika kwa miaka mingi, na pia kutoa onyo kali ili jambo kama hili lisijirudie tena.”
Mvutano wa kisheria unaendelea
Manchester City imesisitiza kutokuwa na hatia na inatarajiwa kutumia kila mbinu ya kisheria kujitetea. Hata hivyo, hali ni ya wasiwasi baada ya Etihad Airways, mmoja wa washirika wao wakuu, kutishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Premier League, wakidai kuwa matokeo ya jopo hilo yameleta athari mbaya kwa sifa yao.
Changamoto kubwa kwa City ni kwamba, ingawa wanapanga kukata rufaa, mamlaka za soka zimepania kuhakikisha kesi hiyo inafika tamati haraka. Bodi ya Premier League, ikiongozwa na Richard Masters, itawasilisha mapendekezo yake ya adhabu mbele ya jopo hilo, huku City wakijaribu kuzuia au kupunguza makali ya adhabu hizo kwa madai kuwa sheria zilizotumika zimeanza kutumika hivi karibuni.
Ikumbukwe kuwa katika kesi ya Everton iliyopita, ambapo klabu hiyo ilipatikana na hatia ya kuzidisha matumizi kwa pauni milioni 19.5, Premier League ilipendekeza kupokonywa pointi 12, ingawa hatimaye walipokonywa pointi 10 ambazo baadaye zilipunguzwa hadi 6 kwenye rufaa. Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa Januari, ambapo uamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya Manchester City utakuwa umewekwa wazi.