Manchester City katika wakati mgumu: Rufaa ya kesi ya FFP kupatiwa ufumbuzi wa haraka
Uamuzi mgumu kwa City
Klabu ya Manchester City inajikuta katika wakati mgumu baada ya ripoti kubainisha kuwa klabu hiyo imepatikana na hatia katika mashtaka 114 kati ya 115 yaliyokuwa yakikabili klabu hiyo kuhusu ukiukwaji wa kanuni za matumizi ya fedha (FFP). Hali hii imezua mjadala mkubwa kuhusu hatima ya klabu hiyo katika Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League).
Kulingana na taarifa zilizotolewa na mwandishi David Ornstein, klabu hiyo sasa inakabiliwa na adhabu kali ambazo zinaweza kujumuisha faini kubwa, kufungiwa kusajili wachezaji, kupunguziwa pointi, kufukuzwa ligi, au hata kuvuliwa mataji ya ligi waliyoyatwaa huko nyuma.
Rufaa na mchakato wa haraka
Ingawa ilitarajiwa kuwa mchakato wa rufaa ungeweza kuchukua muda mrefu, mwandishi Alex Crook ametoa ufafanuzi wa kwanini suala hili linaweza kumalizika kwa haraka zaidi kuliko ilivyodhaniwa awali.
“Kwa kadiri ninavyoelewa, pande zote mbili zilikuwa na siku 14 za kukata rufaa dhidi ya uamuzi wowote uliotolewa na kamisheni huru. Manchester City wanatarajia kukata rufaa, hivyo wana siku 14 za kukamilisha mchakato huo. Baada ya hapo, kamisheni nyingine itaundwa ili kuamua hatima ya rufaa hiyo.”
Crook aliongeza kuwa jambo la msingi ni kwamba klabu hiyo haiwezi kupeleka kesi yao kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), jambo ambalo linazuia kesi hii kusimama kwa miaka mingi kama ilivyokuwa ikihofiwa.
”Hali ni mbaya sana”
Stefan Borson, ambaye aliwahi kuwa mshauri wa kifedha wa Manchester City, ameeleza kuwa klabu hiyo iko katika matatizo makubwa sana. Alisisitiza kuwa tofauti na kesi nyingine kama ya Chelsea ambapo klabu iliweza kufikia mwafaka, Manchester City wamekataa tuhuma zote tangu mwanzo, jambo linalofanya hali kuwa tete.
“Kila kitu kinawezekana na sasa kutakuwa na vurugu kubwa. Manchester City wamekataa kila kitu tangu mwanzo. Wamepitia mchakato ambao huenda umegharimu kiasi cha pauni milioni 100 kwa pande zote mbili, na wamepatikana na hatia katika kila kitu. Wako katika matatizo makubwa sana.”
Kwa sasa, wadau wa soka wanaendelea kusubiri kuona ni hatua zipi zitachukuliwa dhidi ya klabu hiyo, huku kukiwa na shinikizo la kuwekwa hadharani kwa nyaraka zenye kurasa mia kadhaa zinazoelezea uamuzi wa kamisheni hiyo huru. Klabu ya Manchester City inajaribu kuzuia uchapishaji wa ripoti hiyo, lakini wataalamu wanaamini kuwa juhudi hizo huenda zisizae matunda.