Manchester City: Hofu ya 'maafa ya kibiashara' yaweza kuiokoa klabu hiyo dhidi ya kufukuzwa Ligi Kuu
Mgogoro wa kifedha wa Manchester City
Mustakabali wa Manchester City katika Ligi Kuu ya England (Premier League) bado umegubikwa na utata mkubwa. Hii inafuatia uamuzi wa jopo huru kuipata klabu hiyo na hatia ya uvunjifu wa kanuni za kifedha kwa kipindi cha miaka tisa. Uchunguzi umebaini kuwa City walitumia mikataba ya ‘ghushi’ na washirika wa kibiashara ili kuongeza mapato yao kwa kiasi cha zaidi ya pauni milioni 900.
Licha ya hukumu hiyo, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu adhabu stahiki inayopaswa kutolewa. Ingawa kufukuzwa kutoka ligi ni moja ya chaguzi zinazoweza kuchukuliwa na jopo hilo, utekelezaji wa adhabu hiyo unahitaji kura za vilabu 15 kati ya 20 vinavyoshiriki ligi hiyo.
Hofu ya kupoteza mapato makubwa
Uchambuzi wa ndani unaonyesha kuwa klabu nyingi za Ligi Kuu zina wasiwasi mkubwa kuhusu athari za kiuchumi ikiwa City wataondolewa. Maafisa waandamizi kutoka klabu kadhaa wameeleza kuwa uamuzi wa kuifukuza City ungekuwa “maafa ya kibiashara ya kujitakia,” wakiongeza kuwa vilabu vingine vingejiumiza vyenyewe kwa hatua hiyo.
Akizungumza na Sky Sports, mmoja wa watendaji wa klabu hizo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema:
“Kama Manchester City watafukuzwa, hiyo italeta madhara makubwa ya kibiashara kwa kila mtu kwenye ligi, na mwisho wa siku itagharimu vilabu vingine pesa nyingi sana.”
Changamoto za kibiashara na udhamini
Ikiwa City wataondolewa katikati ya msimu, ligi itabaki na timu 19 pekee. Hali hii inatajwa kuwa ingesababisha shinikizo kubwa kutoka kwa watangazaji (broadcasters) wa kimataifa wanaoweza kudai kurejeshewa pesa zao kwa sababu ya kupungua kwa mvuto wa ligi hiyo. Uwepo wa mastaa kama Erling Haaland ni moja ya vivutio vikubwa vinavyoiingizia ligi hiyo mapato makubwa duniani.
Aidha, makampuni ya udhamini yanaweza kujiondoa iwapo klabu yenye mafanikio makubwa zaidi nchini England haitokuwa sehemu ya ligi. Kwa mtazamo huu, baadhi ya vilabu wanaona kuwa kufukuzwa kwa City ni “hatari ambayo haistahili kuchukuliwa.”
Nini kinafuata?
Ingawa maoni ya vilabu hayana nguvu kisheria katika uamuzi wa jopo huru, bado kuna mjadala mkali. Baadhi ya vilabu wanaamini kuwa City lazima wapate adhabu kali, ikiwemo kufukuzwa, ili kulinda heshima na sura ya Ligi Kuu ya England kimataifa.
Kipengele kingine kinachoongeza utata ni hali ya mwenyekiti wa City, Khaldoon Al Mubarak, ambaye imebainika kuwa anashikilia kinga ya kidiplomasia, jambo linalomkinga dhidi ya mashtaka mengi ya kijinai na kisheria nchini Uingereza.
Wakati Manchester City wakitarajiwa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, ulimwengu wa soka unasubiri kwa hamu kuona kama sheria itachukua mkondo wake bila kuathiri maslahi makubwa ya kibiashara ya Premier League.