Manchester City wagomea ofa ya Barcelona kwa Rodri
Mvutano wa bei watawala dili la Rodri
Klabu ya Manchester City imeonyesha msimamo mkali baada ya kuitaja ofa ya awali ya Barcelona kwa ajili ya kiungo wao nyota, Rodri, kuwa ni ndogo sana (derisory). Ingawa klabu hiyo ya Etihad imekubaliana na nia ya mchezaji huyo kurejea nchini kwao Hispania, hawapo tayari kumuuza kwa bei ya kutupa.
Barcelona imetoa ofa ya Euro milioni 45 (takriban Pauni milioni 38) kwa ajili ya huduma ya kiungo huyo, lakini mabingwa hao wa England wameiweka wazi ofa hiyo kando wakisisitiza kuwa wanahitaji kiasi kisichopungua Euro milioni 80 (takriban Pauni milioni 68.5) ili kuruhusu dili hilo kukamilika.
Rodri atakiwa kurejea City
Wakati mazungumzo yakiendelea, Manchester City wametoa maelekezo kwa Rodri kurejea klabuni hapo ili kuendelea na matibabu yake ya mgongo, akitoka kufanyiwa upasuaji mdogo. Klabu hiyo imesisitiza kuwa mchezaji huyo atabaki jijini Manchester hadi hapo ofa inayokidhi mahitaji yao itakapowasilishwa.
Inafahamika kuwa Rodri ana mkataba uliosalia na mwaka mmoja pekee, jambo ambalo limeibua tetesi kuwa City wanaweza kumshawishi kusaini mkataba mpya iwapo Barcelona watashindwa kufikia dau lao. Licha ya matatizo ya kifedha yanayoikabili Barcelona, taarifa kutoka kwa wachambuzi wa soka zinaeleza kuwa miamba hiyo ya Camp Nou bado ina matumaini ya kufanikiwa na inatarajiwa kuwasilisha ofa nyingine hivi karibuni.
City wajipanga na mrithi
Katika kuhakikisha hawapotezi makali kwenye safu yao ya kiungo, Manchester City wanaonekana kujiandaa na maisha baada ya Rodri. Taarifa za ndani zinaonyesha kuwa klabu hiyo iko katika hatua za mwisho za mazungumzo kumsajili kiungo kijana, Ayyoub Bouaddi kutoka klabu ya Lille ya Ufaransa.
“Manchester City wanatarajiwa kukamilisha maelezo yote ya dili la Ayyoub Bouaddi hivi karibuni, kabla ya kuelekeza nguvu zao kwenye usajili mwingine,” chanzo cha karibu na klabu hiyo kimesema.
Hali hii inaashiria kuwa City hawapo tayari kubabaishwa na presha ya soko, na wako makini kuhakikisha kikosi cha Pep Guardiola kinabaki imara kwa ajili ya msimu ujao.