Manchester City wamuotea Alexis Mac Allister kuchukua nafasi ya Rodri
Hofu ya kumkosa Rodri inaipeleka Man City kwa Mac Allister
Klabu ya Manchester City imeanza kuchukua hatua za dharura kujiimarisha katika dirisha la usajili huku kukizuka hofu ya kumpoteza kiungo wao tegemeo, Rodri. Taarifa za karibuni zinaeleza kuwa mabingwa hao wa England wameanza kuwasiliana na wawakilishi wa kiungo wa Liverpool, Alexis Mac Allister, wakimwona kama chaguo sahihi kuziba pengo hilo.
Rodri, ambaye mkataba wake na Etihad Stadium unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, bado haonyeshi dalili za kuongeza mkataba mpya. Hali hii imeifanya klabu hiyo kuanza kutafuta mbadala wa haraka endapo staa huyo atatimka kuelekea nchini Hispania.
Ujumbe kutoka kwa mdau wa usajili
Kulingana na ripoti ya mwandishi Matt Thielen, Manchester City wamemweka Mac Allister kwenye orodha yao ya wachezaji wanaowahitaji kwa ajili ya msimu ujao. Thielen alithibitisha kupitia mtandao wa X:
“Manchester City wamefanya mawasiliano na kambi ya Alexis Mac Allister ili kuchunguza uwezekano wa kumnunua kiungo huyo wa Liverpool. Mac Allister yumo kwenye orodha fupi ya wachezaji wanaolengwa na City iwapo Rodri ataondoka klabuni hapo.”
Mac Allister, mwenye umri wa miaka 27, ameonyesha kiwango bora tangu ajiunge na Liverpool mwaka 2023, akifanikiwa kutwaa ubingwa wa Premier League na EFL Cup. Uzoefu wake na uwezo wake wa kumudu eneo la kiungo unatazamwa kama sifa kuu inayomfanya City kumvizia.
Rodri anapendelea Barcelona kuliko Real Madrid
Wakati huohuo, mustakabali wa Rodri unaendelea kuteka vichwa vya habari. Awali, Real Madrid walikuwa wakimwania kwa karibu kiungo huyo, hata hivyo, ripoti zinaeleza kuwa mchezaji huyo ameweka wazi kuwa Barcelona ndiyo sehemu anayopendelea zaidi kuitumikia.
Inadaiwa kuwa Real Madrid wameamua kujiondoa kabisa katika mbio za kumsajili Rodri baada ya kupata taarifa za msimamo wake. Viongozi wa Madrid wamejenga utamaduni wa kutaka wachezaji ambao wako tayari kujitoa kwa asilimia mia moja kwa klabu hiyo, hivyo wameamua kuachana na mpango huo.
Kwa sasa, mashabiki wa soka wanasubiri kuona kama kweli Manchester City watafanikiwa kumshawishi Mac Allister kuondoka Anfield, hatua ambayo ingekuwa miongoni mwa usajili wa kushangaza zaidi katika historia ya hivi karibuni ya Ligi Kuu ya England.