Skip to content

Manchester United bado wanapambana kumbakiza kinda JJ Gabriel

SokaNews
Updated: Published: Ijumaa, 18 Septemba 2026 · 2 min read
manchesterunited jjgabriel fabrizioromano sokalavijana usajili realmadrid
Manchester United bado wanapambana kumbakiza kinda JJ Gabriel

Hatima ya JJ Gabriel bado ni kitendawili Old Trafford

Klabu ya Manchester United bado inafanya jitihada za mwisho kuhakikisha inambakiza kinda wake mwenye kipaji kikubwa, JJ Gabriel, baada ya taarifa kushtua ulimwengu wa soka kwamba kijana huyo ameomba kuondoka klabuni hapo.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 15, ambaye anatarajiwa kutimiza miaka 16 mwezi ujao, anatajwa kuwa miongoni mwa vipaji bora zaidi kuwahi kushuhudiwa katika akademi ya Manchester United. Hali imekuwa mbaya zaidi baada ya ripoti kubainisha kuwa ametoa taarifa rasmi ya kutaka kuvunja mkataba wake na kuwa mchezaji huru.

United hawataki kulazimisha mambo

Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amebainisha kuwa uongozi wa Manchester United bado umegubikwa na mshangao kutokana na uamuzi huo wa ghafla. Licha ya hayo, klabu imesisitiza kuwa haitaki kutumia nguvu kumbakiza mchezaji asiyekuwa na furaha.

“United hawataki kulazimisha mtu yeyote. Ni wazi wanataka kumbakiza kijana huyo na hawataki kumpoteza mmoja wa vipaji bora duniani, lakini kwa wakati uleule, hawataki kulazimisha mazingira,” alisema Romano.

Romano aliongeza kuwa klabu hiyo inajipanga kufanya mazungumzo ya ngazi za juu, yakihusisha watu muhimu ndani ya uongozi wa klabu hiyo, ikiwemo Sir Jim Ratcliffe, ili kutatua mgogoro huo na kuona kama kuna nafasi yoyote ya kufika mwafaka.

Uhispania ndio njia panda?

Kuhusu hatima ya kijana huyo iwapo ataondoka Old Trafford, Romano amedokeza kuwa nchi ya Uhispania ndiyo inayopewa nafasi kubwa zaidi kuwa nyumbani kwa kinda huyo. Klabu za Real Madrid na Barcelona zimetajwa kuwa miongoni mwa zinazofuatilia kwa karibu maendeleo ya kinda huyo.

“Kwa sasa, ukiuliza ni wapi anaelekea, Real Madrid wanaonekana kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kumnasa JJ Gabriel. Lakini hata Barcelona nao wapo kwenye mawasiliano,” aliongeza Romano.

Inafahamika kuwa klabu nyingi kubwa barani Ulaya, zikiwemo Bayern Munich na PSG, zimeonyesha nia ya kutaka huduma ya kinda huyo. Hata hivyo, kwa sasa, Manchester United bado hawajakata tamaa na wanaendelea na jitihada zao za kumshawishi mchezaji huyo na familia yake ili aendelee kubaki katika klabu hiyo aliyoanza kuichezea tangu akiwa na umri wa miaka 11.