Manchester United yafunga milango kwa Carlos Baleba, Newcastle wagoma kumuuza Lewis Hall
United yafunga mlango kwa Baleba
Klabu ya Manchester United imethibitisha kuwa haitaendelea na harakati za kumsajili kiungo wa Brighton, Carlos Baleba, katika dirisha hili la usajili la majira ya joto. Uamuzi huu umekuja baada ya taarifa za kuaminika kuonyesha kuwa kiungo huyo anakabiliwa na majeraha ambayo yatafanya akose kuanza kwa msimu wa 2026/27.
Mwandishi maarufu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amethibitisha kupitia chaneli yake ya YouTube kuwa majeraha hayo yamefanya hali kuwa ngumu kwa mashetani wekundu hao wa Old Trafford.
“Majeraha ya Carlos Baleba yanafanya mambo kuwa magumu zaidi. Hivyo, kwa wakati huu, Manchester United haitaendelea na dili la kumsajili Carlos Baleba,” alisema Romano.
Hapo awali, Baleba alikuwa akihusishwa kwa karibu na United huku kukiwa na taarifa kuwa bei yake imeshuka hadi kufikia takriban paundi milioni 50, tofauti na msimu uliopita ambapo thamani yake ilikuwa juu sana. Licha ya jina lake kuonekana kama chaguo sahihi la kuimarisha safu ya kiungo, United imeonekana kutotaka kubahatisha na mchezaji ambaye hajawa fiti.
Newcastle yagomea ofa ya Lewis Hall
Katika upande mwingine wa uwanja, Manchester United wamekutana na kizuizi kikubwa katika azma yao ya kumsajili beki wa kushoto wa Newcastle United, Lewis Hall. United wamekuwa wakimfuatilia mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 21 kwa muda mrefu ili kuongeza nguvu katika safu yao ya ulinzi.
Hata hivyo, Newcastle wamekuwa imara katika msimamo wao. Mwandishi Keith Downie wa Sky Sports amethibitisha kuwa Newcastle wametoa majibu rasmi kwa Manchester United kuwa mchezaji huyo hauzwi.
“Newcastle United wameiambia Manchester United kuwa beki wa kushoto Lewis Hall hauzwi msimu huu, baada ya uchunguzi wao wa awali kukataliwa,” alifafanua Downie.
Romano ameongeza kuwa ingawa Hall ni mchezaji ambaye yupo kwenye orodha ya muda mrefu ya United, Newcastle wana mipango naye na wao wenyewe wapo sokoni wakitafuta beki mwingine wa kuongeza kikosi chao.
Hadi sasa, Manchester United, chini ya uongozi wa INEOS, wamefanikiwa kuwasajili Andrey Santos na Youri Tielemans ili kuimarisha safu yao ya kiungo. Inatarajiwa kuwa klabu hiyo haitafanya usajili wa dharura wa kiungo wa tatu kama ambavyo ilikuwa ikipendekezwa awali, badala yake wataangalia wachezaji sahihi watakaopatikana kwa bei inayofaa.