Skip to content

Manchester United hatarini kumpoteza kinda JJ Gabriel, Real Madrid wapo mbioni kumnasa

SokaNews
Updated: Published: Alhamisi, 17 Septemba 2026 · 2 min read
manchesterunited jjgabriel realmadrid usajili premierleague chipukizi
Manchester United hatarini kumpoteza kinda JJ Gabriel, Real Madrid wapo mbioni kumnasa

Hatima ya JJ Gabriel Man Utd yafahamika

Manchester United wako katika wakati mgumu baada ya kinda wao mwenye kipaji cha hali ya juu, JJ Gabriel, kuonyesha nia ya kutaka kuondoka klabuni hapo. Kinda huyu mwenye umri wa miaka 15 amekuwa gumzo kutokana na kiwango chake bora kwenye soka la vijana, jambo ambalo limefanya klabu kubwa barani Ulaya kuanza kummezea mate.

Taarifa zinaeleza kuwa mchezaji huyo na wawakilishi wake wamekuwa hawana furaha ndani ya Old Trafford. Inaonekana sababu kubwa ya uamuzi huu ni kutaka kupata nafasi zaidi katika kikosi cha kwanza, jambo ambalo linaonekana kusuasua kulingana na matarajio yao.

Real Madrid mbele katika mbio za kumsajili

Ingawa klabu nyingi kubwa zinamnyatia kinda huyu, Real Madrid wameonekana kuwa mstari wa mbele zaidi. Mchambuzi wa michezo, Ben Jacobs, amedai kuwa miamba hiyo ya Hispania ina nafasi nzuri ya kumsajili Gabriel.

“Real Madrid ndio wanaongoza mbio hizi na ndio klabu anayoipendelea, lakini Barcelona nao wanafanya jitihada za chini kwa chini kuhakikisha wanamsajili,” alisema Jacobs.

Sababu kubwa inayotajwa kuifanya Real Madrid kuwa chaguo la kwanza la Gabriel ni mfumo wao wa akademi, uwepo wa timu yao ya Castilla inayotoa uzoefu wa kulipwa, na imani ya mchezaji huyo kwa kocha wa sasa wa timu hiyo.

United wajaribu kuokoa jahazi

Licha ya taarifa za kuondoka kwake kuwa na uzito mkubwa, klabu ya Manchester United bado inafanya juhudi za mwisho kumshawishi kinda huyo abadili maamuzi. Hata hivyo, hali halisi uwanja wa mazoezi wa Carrington inaonyesha mambo yameiva kuelekea mlango wa kutokea. Gabriel hajaonekana uwanjani hapo tangu alipofunga hat-trick katika mechi ya UEFA Youth League wiki iliyopita.

Baadhi ya wadau wa soka wanaamini kuwa kupoteza kipaji hiki ni hasara kubwa kwa United, huku kukiwa na hofu kuwa huenda wakawa wanapoteza mchezaji ambaye thamani yake inaweza kufika Pauni milioni 100 hapo baadaye.

Maoni ya Neville kuhusu usimamizi wa vipaji

Kuhusu hali hiyo, gwiji wa Manchester United, Gary Neville, amekosoa namna kinda huyo anavyoshughulikiwa. Akilinganisha na jinsi klabu nyingine zinavyolinda vipaji vyao, Neville alisema:

“Unataka kujaribu kuzima moto, sivyo? Hutaki kuongeza mafuta kwenye moto pale unapokuwa na kinda kama huyu. Kumbuka Max Dowman (wa Arsenal), walikataa kumpa mahojiano baada ya mchezo ili amrudishe haraka vyumbani, na Jumatatu alikuwa shuleni kama kawaida. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kulinda chipukizi.”

Kwa sasa, ni suala la kusubiri kuona kama United watafanikiwa kumshawishi kijana huyo kubaki, au kama atafuata nyayo za kujiunga na miamba ya Ulaya kama Real Madrid, Barcelona, PSG au Bayern Munich.