Manchester United katika mazungumzo ya kumsajili Andrey Santos kutoka Chelsea
Manchester United imeonyesha dhamira ya kuimarisha eneo lake la kiungo katika dirisha hili la usajili, ambapo sasa imeripotiwa kuwa kwenye hatua nzuri za kufikia makubaliano na Chelsea kwa ajili ya kumsajili kiungo Andrey Santos.
Taarifa kutoka nchini Uingereza zinaeleza kuwa klabu hizo mbili zimeanza mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu uhamisho wa nyota huyo raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 22. Inasemekana Chelsea inahitaji kitita cha pauni milioni 50 ili kumwachia kiungo huyo.
Umuhimu wa usajili huu kwa United
Mahitaji ya Manchester United ya kuongeza kiungo mpya yamechochewa na mabadiliko katika kikosi chao. Mkongwe Casemiro ameondoka klabuni hapo, huku Manuel Ugarte akitarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha. Hali hii imemlazimu kocha Michael Carrick na uongozi wa INEOS kuhakikisha wanapata mbadala wa uhakika ili kuimarisha safu hiyo kuelekea msimu mpya ambapo United itashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ingawa tayari United imefikia makubaliano na Atalanta kwa ajili ya kumnasa Ederson Silva, inaonekana bado wanahitaji mtu mwingine ili kuongeza kina katika kikosi chao.
Chelsea wapo tayari kuuza
Awali, kulikuwa na sintofahamu ikiwa Chelsea wangekuwa tayari kumwachia kijana huyu, lakini taarifa za kuaminika zinaonyesha kuwa Andrey Santos haonekani kuwa mchezaji ‘asiyeguswa’ kikosini. Mchambuzi wa mambo ya usajili Fabrizio Romano alibainisha kuwa:
Chelsea hawamchukuli ‘untouchable’ Andrey Santos. Hivyo, kama Man Utd wakija na ofa nzuri mezani, wana nafasi ya kumsajili. Kwa upande wa Chelsea, kuna uwezekano wa yeye kuondoka msimu huu kama ofa ya kuridhisha itatolewa.
Historia ya uhusiano na mchezaji
Uhusiano kati ya Manchester United na wawakilishi wa Santos si jambo geni. Inakumbukwa kuwa mapema mwaka huu, klabu hiyo ilifanya mazungumzo kadhaa na mawakala wa kiungo huyo, ambaye anashirikiana na wawakilishi sawa na Bruno Guimaraes. Lengo lilikuwa ni kuelewa mazingira ya kumpata mchezaji huyo, na sasa mazungumzo hayo yamepanda daraja na kufikia ngazi ya klabu.
Ikiwa pande zote zitafikia muafaka, huu utakuwa usajili mwingine muhimu kwa Michael Carrick katika jitihada zake za kuijenga upya Manchester United na kuifanya kuwa tishio tena kwenye ligi kuu ya England na barani Ulaya.