Manchester United kuelekea kumsajili Adrien Truffert
Utafutaji wa beki wa kushoto unaendelea
Manchester United inaonekana kuwa na mikakati mipya ya kuimarisha safu yake ya ulinzi, hasa eneo la beki wa kushoto. Baada ya jitihada zao za kumsajili Lewis Hall kutoka Newcastle United kugonga mwamba katika dirisha la usajili lililopita, sasa klabu hiyo inaelezwa kumweka Adrien Truffert wa Bournemouth kwenye rada zao.
Taarifa kutoka kwa mwandishi mahiri David Ornstein zinaeleza kuwa, baada ya Newcastle kusisitiza kuwa Lewis Hall hauzwi, United iliamua kusitisha mipango hiyo kwa muda. Hata hivyo, hali imekuwa ngumu zaidi kwa sasa kwani Hall ameshasaini mkataba mpya na Newcastle ambao hauna kipengele cha kuruhusu kuvunjwa kwa mkataba (release clause), jambo linalofanya uhamisho huo kuwa mgumu sana katika siku za usoni.
Truffert, chaguo sahihi kwa United?
Kufuatia hali hiyo, United imeanza kutathmini machaguo mengine kwa ajili ya dirisha la usajili la mwaka 2027. Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa ni Jorge Salinas (Racing Santander), Joaquin Seys (Club Brugge), David Raum (RB Leipzig), na Alejandro Balde (Barcelona). Hata hivyo, jina la Adrien Truffert linaonekana kupata nafasi kubwa.
Akizungumza kupitia The Athletic FC Podcast, Ornstein alidokeza kuwa klabu nyingi zitakuwa na uhitaji wa beki wa kushoto hivi karibuni. Kuhusu Truffert, alisema:
“Truffert ana umri mzuri na sifa ambazo klabu kubwa zinazitaka. Nasikia thamani yake inaweza kuwa karibu pauni milioni 60, na kuna uwezekano wa dili kufanyika msimu ujao. Ni mchezaji ninayemwona ana uwezo wa kucheza katika klabu yoyote kubwa duniani.”
Maoni ya wataalamu
Kiwango cha beki huyo wa Kifaransa kimevutia wengi katika Ligi Kuu ya England. Mchambuzi wa talkSPORT, Jason Cundy, alimwagia sifa lukuki mchezaji huyo hivi karibuni baada ya Bournemouth kutoa sare ya 2-2 dhidi ya Newcastle.
“Ni mchezaji mahiri sana. Nadhani anaweza kuwa beki bora wa kushoto nchini kwa sasa. Truffert atapata uhamisho mkubwa, na unajua nani anapaswa kumsajili? Manchester United. Amekuwa na kiwango bora tangu msimu uliopita na ni beki mzuri kweli,” alisema Cundy.
Inaonekana Bournemouth watahitaji dau kubwa ili kumwachia nyota huyo, lakini kutokana na mahitaji ya kikosi cha Michael Carrick, mazungumzo kuhusu mchezaji huyo yanaweza kuwa moja ya habari kubwa katika dirisha la usajili lijalo.