Manchester United kutarajia mgao mnono kupitia dili la Mason Greenwood kwenda Fenerbahce
Man United kusubiri faida kupitia dili la Greenwood
Klabu ya Manchester United iko katika nafasi nzuri ya kupata kiasi kikubwa cha pesa kutokana na hatua ya mshambuliaji wao wa zamani, Mason Greenwood, kukaribia kutimkia nchini Uturuki kujiunga na klabu ya Fenerbahce.
Greenwood, ambaye kwa sasa anachezea Olympique de Marseille ya Ufaransa, amekuwa kwenye mvutano na viongozi wa klabu hiyo, jambo lililochochea mlango wa kuondoka kwake kufunguka katika dirisha hili la usajili. Hali hii imeifanya Fenerbahce kujitokeza kwa nguvu kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24.
Makubaliano yanakaribia kukamilika
Ripoti kutoka nchini Ufaransa zimebainisha kuwa Fenerbahce wako mbioni kufikia makubaliano na Marseille. Awali, ofa ya Euro milioni 30 ilikataliwa na Marseille, lakini klabu hiyo ya Uturuki imeongeza dau ili kukidhi matakwa ya Wafaransa hao.
Mwandishi wa habari za michezo, Nicolo Schira, amethibitisha kuwa Greenwood mwenyewe ameshafungua mlango wa kujiunga na Fenerbahce baada ya kupewa ofa ya mshahara wa Euro milioni 8 kwa mwaka pamoja na marupurupu mengine kwenye mkataba wa muda mrefu.
Mason Greenwood amefungua mlango wa kujiunga na Fenerbahce na ametoa ridhaa yake baada ya ofa kubwa iliyowasilishwa na klabu hiyo ya Uturuki katika saa za hivi karibuni, alisema Schira.
Man United watafaidika vipi?
Wakati United walipomuuza Greenwood kwenda Marseille kwa kiasi cha takriban Euro milioni 26, walihakikisha wanaingiza kipengele cha kupata asilimia 50 ya mauzo yake ya baadaye.
Ikiwa Marseille itafanikiwa kupata dau la Euro milioni 55 (takriban Pauni milioni 47) kama wanavyotaka, Manchester United itapata kiasi cha karibu Pauni milioni 23.5 kupitia kipengele hicho cha ‘sell-on clause’. Huu unatazamwa kama mchango mkubwa wa kiuchumi kwa mashetani wekundu hao ambao wanaendelea na mipango yao ya kusuka upya kikosi.
Greenwood amekuwa na kiwango bora ndani ya Marseille, akifunga mabao 48 na kutoa pasi 17 za mabao katika michezo 81 aliyoichezea timu hiyo kwa kipindi cha misimu miwili. Hata hivyo, kutokana na kutoelewana na uongozi wa klabu, safari yake ya kuelekea Uturuki inaonekana kuwa ndiyo hatua inayofuata katika maisha yake ya soka.