Manchester United wamsaka mrithi wa JJ Gabriel nchini Norway
United kwenye wakati mgumu kuhusu JJ Gabriel
Klabu ya Manchester United inapita katika kipindi kigumu kuhusiana na hatima ya kinda wake hatari, JJ Gabriel, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa vipaji bora zaidi kuwahi kutokea katika akademi ya klabu hiyo. Kinda huyo mwenye umri wa miaka 15, anayotarajia kufikisha miaka 16 mwezi Oktoba, amekuwa gumzo baada ya kuonyesha uwezo mkubwa, ikiwemo kufunga mabao matatu (hat-trick) katika mchezo wake wa kwanza wa UEFA Youth League.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa mchezaji huyo amewasilisha ombi la kutaka kuondoka Old Trafford, hali iliyozua mshtuko mkubwa ndani ya uongozi wa klabu hiyo. Fabrizio Romano amedai kuwa hali hiyo ni ngumu, huku klabu kubwa kama Chelsea, Real Madrid, na Barcelona zikihusishwa na jitihada za kumshawishi kinda huyo.
“Ni hali ngumu sana kwa kila upande. Tunapozungumzia kipaji kama JJ Gabriel, bila shaka unataka kimbakize. Ni mchezaji ambaye tumekuwa tukimfuatilia kwa miaka mingi na kumuona kama mmoja wa vipaji bora zaidi kuwahi kuonekana klabuni,” alisema Romano.
United watazama Norway kwa ajili ya Rajkovic
Licha ya jitihada za viongozi wa United, akiwemo Sir Jim Ratcliffe, kujaribu kuweka mambo sawa na kinda huyo ambaye kwa sasa amesitisha mazoezi, klabu imeanza kuangalia mbadala wake. Taarifa kutoka nchini Norway zinaeleza kuwa United wametuma maofisa wao kwenda kumtazama kinda mwingine hatari, Gabriel Rajkovic, anayekipiga katika klabu ya Valerenga.
Rajkovic, ambaye amekuwa akiishabikia Manchester United tangu utotoni, amekuwa akivutia macho ya mawakala wengi. Hata hivyo, klabu ya Valerenga haina haraka ya kumuuza staa wake huyo chipukizi, ambapo inatajwa kuwa klabu hiyo itahitaji dau lisilopungua paundi milioni 16 ili kumwachia kijana huyo.
Nini kinafuata?
Kuelekea siku za usoni, Manchester United wanasisitiza kuwa hawataki kulazimisha mchezaji yeyote kubaki ikiwa hataki, lakini wataendelea na mazungumzo na familia pamoja na mawakala wa JJ Gabriel ili kuona kama kuna nafasi ya kutatua mgogoro huo.
Wakati huo huo, kufuatiliwa kwa Rajkovic ni ishara kuwa United wanajipanga vyema kuhakikisha akademi yao inabaki na makali, iwe kwa kumshawishi JJ Gabriel kubaki au kwa kuleta vipaji vipya kutoka nje ya Uingereza.