Manchester United wabadili gia angani baada ya kupoteza nafasi ya kumsajili Mateus Fernandes
United yajipanga upya sokoni
Kikosi cha Manchester United kimepata pigo katika dirisha hili la usajili baada ya kushindwa kumnasa kiungo machachari, Mateus Fernandes kutoka West Ham United. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 sasa anajiunga rasmi na Tottenham Hotspur, jambo lililowalazimu ‘Mashetani Wekundu’ hao kutafuta mbadala haraka.
Tottenham imefanikiwa kumpata nyota huyo baada ya kutoa kitita cha paundi milioni 85, kiasi ambacho Manchester United waliona ni kikubwa sana na kutokua tayari kukilipa. Mwandishi David Ornstein amethibitisha kuwa dau la Spurs ndilo lililokuwa la juu zaidi na kumfanya Fernandes kuchagua kuelekea kaskazini mwa London.
Kwa nini Fernandes amechagua Spurs?
Ripoti za ndani zinaeleza kuwa uamuzi wa Fernandes haukutokana na maslahi ya fedha pekee. Ingawa ofa ya Tottenham ilikuwa nzuri, kiungo huyo amevutiwa zaidi na mradi wa kocha Roberto De Zerbi.
“Fernandes alimchagua Tottenham kutokana na imani yake katika maono ya Roberto De Zerbi kwa klabu hiyo. Suala halikuwa tu kwenda kwa anayetoa fedha nyingi zaidi, bali ni mwelekeo wa mradi na nafasi ya kuendelea kuishi jijini London,” imeeleza ripoti hiyo.
Alex Scott ndiye mlengwa mpya
Baada ya mpango wa Fernandes kufeli, Manchester United sasa wamegeuza macho yao kwa kiungo wa Bournemouth, Alex Scott. Mwandishi wa habari za michezo, Ben Jacobs, amedokeza kuwa klabu hiyo inatafuta njia za kuanza mazungumzo kuhusu mchezaji huyo.
Hata hivyo, usajili wa Scott hautakuwa rahisi kwani Bournemouth inamthamini kwa takriban paundi milioni 80 na inataka kumuongezea mkataba mpya wenye kipengele cha kuuzwa. Klabu nyingine kubwa kama Arsenal, Manchester City na Chelsea pia zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya kiungo huyo.
Nani wengine wapo kwenye rada ya United?
Licha ya Alex Scott, Manchester United bado ina orodha ndefu ya viungo wanaowavizia ili kuimarisha kikosi cha kocha Michael Carrick. Majina yanayotajwa ni pamoja na Aurelien Tchouaméni na Carlos Baleba. Vilevile, klabu hiyo inamvulia kofia Sandro Tonali, ingawa watalazimika kusubiri gharama za usajili wake zishuke ili waweze kufanya biashara.
Ni dhahiri kuwa safu ya kiungo ni kipaumbele cha United msimu huu, hasa baada ya kupata changamoto ya majeraha kwa Manuel Ugarte, jambo ambalo limefanya mchakato wa usajili kuwa mgumu zaidi kuliko ilivyotarajiwa.