Manchester United yabadili gia angani, yataja viungo watatu wapya baada ya dili la Ederson kufeli
Mabadiliko ya ghafla Old Trafford
Klabu ya Manchester United imeamua kubadili gia angani kwenye harakati zake za kuimarisha eneo la kiungo kwa msimu ujao. Baada ya mpango wa kumsajili Ederson Silva kutoka Atalanta kukwama, mabosi wa INEOS wameelekeza nguvu zao kwenye orodha mpya ya wachezaji watatu ambao wamepangwa kusajiliwa wawili kati yao.
Taarifa kutoka nchini Uingereza zinathibitisha kuwa Manchester United imepiga hodi kwa Chelsea na kufikia makubaliano ya kumnasa Andrey Santos kwa kitita cha pauni milioni 50, hatua inayoongeza nguvu kwenye safu hiyo ya kati chini ya kocha Michael Carrick, ambaye msimu ujao atawaongoza vijana hao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Dili la Ederson lafika mwisho
Ndoto ya Manchester United kumpata Ederson ilionekana kukamilika baada ya pande zote mbili kufikia muafaka, hata hivyo, mambo yamebadilika. Mwandishi Fabrizio Romano amethibitisha kuwa United imetuma mawasiliano rasmi kwa Atalanta kuvunja makubaliano hayo.
Sababu kubwa ya uamuzi huo ni matokeo ya vipimo vya afya. Ingawa Atalanta wanashikilia msimamo kuwa kiungo huyo yuko fiti kwa asilimia 100 na alicheza Kombe la Dunia akiwa na Brazil bila shida, Manchester United iliona kuna haja ya kufanya vipimo zaidi ambavyo hatimaye vilisababisha viongozi wa Old Trafford kuvunja mkataba huo.
Orodha ya viungo watatu wanaowaniwa
Kufuatia kuporomoka kwa dili la Ederson, sasa Manchester United inatafuta viungo wengine wawili wa kuungana na Santos. Kwa mujibu wa mwandishi Eduardo Burgos, klabu hiyo imeweka wazi orodha ya wachezaji watatu ambao wanafuatiliwa kwa karibu:
- Manu Kone: Kiungo wa AS Roma ambaye anang’ara katika michuano ya Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa.
- Alex Scott: Nyota wa Bournemouth ambaye anatajwa kama mmoja wa viungo bora wenye umri mdogo na uwezo mkubwa wa kukua ndani ya Premier League.
- Ayyoub Bouaddi: Kijana mwenye umri wa miaka 18 anayekipiga Lille, ambaye amevutia macho ya wachunguzi wa United kutokana na kiwango chake bora kwenye Kombe la Dunia akiwa na Morocco.
Changamoto za usajili
Kila mchezaji kwenye orodha hiyo ana changamoto zake. Wakati AS Roma wakiwa tayari kumuuza Kone ili kuongeza thamani yake kufuatia michuano ya Kombe la Dunia, hali ni tofauti kwa Bournemouth ambao hawana haraka ya kumuuza Alex Scott kutokana na umuhimu wake.
Kwa upande wa kijana Bouaddi, klabu yake ya Lille imeweka bayana kuwa wako tayari kufanya biashara, lakini wanataka mchezaji huyo abaki kwa mkopo kwanza msimu ujao kabla ya kujiunga rasmi na klabu mpya. Manchester United sasa inatakiwa kufanya maamuzi magumu kuchagua wawili kati ya hawa ili kukamilisha kikosi cha Michael Carrick kwa ajili ya changamoto za msimu ujao.