Manchester United yafungua milango kwa Marcus Rashford
Hatma ya Rashford Old Trafford
Klabu ya Manchester United imeonekana kubadili mwelekeo kuhusu mustakabali wa mshambuliaji wake, Marcus Rashford, baada ya kurejea kikosini kufuatia msimu mmoja wa mkopo nchini Hispania. Taarifa za ndani zinaeleza kuwa klabu hiyo sasa inajiandaa kumuunganisha tena mchezaji huyo na kikosi cha kocha Michael Carrick.
Rashford alitumia msimu uliopita kwa mkopo katika klabu ya Barcelona, ambapo mkataba wake ulikuwa na kipengele cha kumnunua jumla kwa kiasi cha Euro milioni 30. Hata hivyo, mabingwa hao wa La Liga waliamua kutotekeleza kipengele hicho, jambo lililopelekea mjadala mpya kuhusu hatma ya mchezaji huyo.
Mazungumzo ya chanya
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amebainisha kuwa kumekuwa na mabadiliko ya kimtazamo kati ya pande zote mbili. Katika mkutano wa hivi karibuni kati ya wawakilishi wa mchezaji huyo na uongozi wa United, kumekuwa na maelewano mazuri.
“Marcus Rashford sasa anaonyesha ishara chanya kwa Manchester United kuhusu uwezekano wa kusalia klabuni. Dirisha la usajili bado lina wiki nane, hivyo hatuwezi kusema kwa asilimia 100 atabaki, lakini Rashford hafungi milango ya kurejea kikosini na kushiriki maandalizi ya msimu mpya chini ya Michael Carrick.”
Maandalizi ya kurudi kikosini
Ripoti nyingine zinaeleza kuwa Mkurugenzi wa Soka wa klabu hiyo, Jason Wilcox, amewapa maelekezo wafanyakazi wa klabu kuhakikisha wako tayari iwapo Rashford atabaki Old Trafford. Hatua hii imelenga kuhakikisha kuwa kocha Carrick anakuwa na mpango madhubuti wa kumjumuisha mshambuliaji huyo katika mfumo wake wa kwanza.
Licha ya kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa kubaki, klabu bado haijafunga milango ya mauzo endapo kutatokea ofa nzuri kwa pande zote mbili. Kwa sasa, United inamtazama Rashford kama mchezaji muhimu ambaye anaweza kutoa mchango mkubwa kikosini msimu ujao, huku ikisubiri mwenendo wa soko la usajili.
Hali hii inadhihirisha kuwa United haitaki kushikwa na butwaa, na badala yake inajipanga vyema ili kuhakikisha kuwa mchezaji huyo anaweza kurejesha makali yake ndani ya jezi nyekundu msimu ujao.