Skip to content

Manchester United yagomea ofa ya Juventus kwa Joshua Zirkzee

SokaNews
Updated: Published: Jumatatu, 31 Agosti 2026 · 2 min read
manchesterunited joshuazirkzee juventus victorosimhen usajili premierleague
Manchester United yagomea ofa ya Juventus kwa Joshua Zirkzee

Mvutano wa usajili wa Zirkzee

Klabu ya Manchester United imethibitisha kuwa na msimamo mkali katika siku hizi za mwisho za dirisha la usajili baada ya kukataa ofa ya kwanza ya Juventus kwa ajili ya mshambuliaji wao, Joshua Zirkzee.

Taarifa kutoka nchini Italia kupitia mwandishi Gianluca Di Marzio zinaeleza kuwa Juventus iliwasilisha ofa ya mkopo yenye thamani ya takriban Euro milioni 2.5, ikiwa na kipengele cha kumnunua jumla mchezaji huyo kwa Euro milioni 30.

Hata hivyo, Manchester United inaonekana kutokubaliana na dau hilo. Mabingwa hao wa zamani wa England wanataka ofa ya jumla isiyopungua Euro milioni 35 ili waweze kumwachia mshambuliaji huyo. Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yanaendelea huku saa zikiyoyoma kuelekea kufungwa kwa dirisha la usajili siku ya Jumanne.

Kabla ya ofa hiyo ya Juventus, Zirkzee alihusishwa na taarifa za kujiunga na Fiorentina, lakini mchezaji huyo aligomea dili hilo na sasa hatima yake iko mikononi mwa klabu yake na ofa yoyote itakayokidhi vigezo vyao.

Victor Osimhen anatajwa kama mbadala

Wakati kukiwa na sintofahamu ya Zirkzee, jina la staa wa kimataifa wa Nigeria, Victor Osimhen, limeendelea kutawala vichwa vya habari kama mbadala sahihi wa kuimarisha safu ya ushambuliaji ya ‘Mashetani Wekundu’ hao.

Gwiji wa zamani wa Manchester United, Louis Saha, amedai kuwa mshambuliaji huyo anayeandamwa na Arsenal, ana mapenzi makubwa na United na bado anasubiri nafasi ya kutua Old Trafford.

“Najua kwa hakika kuwa Victor Osimhen ni shabiki wa Manchester United. Anaikubali sana klabu hii. Nimeona katika macho yake, athari kubwa ambayo klabu hii inayo kwake, na anajua mchango ambao anaweza kuutoa katika timu hii,” alisema Saha.

Saha anaamini kuwa Osimhen ana sifa zote za kuwa mshambuliaji kinara wa United kutokana na rekodi yake ya kufunga mabao 20 kila msimu na nguvu zake za kimwili ambazo ni muhimu katika ligi ya England.

“Osimhen anaweza kuwa kama Bruno Fernandes. Ana tabia ya kutokukata tamaa, anafanya kazi kwa bidii, na ni mchezaji asiyetabirika. Manchester United inachotakiwa kufanya ni kuunganisha dots tu ili kufanikisha dili hili,” aliongeza Saha.

Kuelekea saa za mwisho za dirisha la usajili, mashabiki wa United wanaendelea kusubiri kuona kama uongozi wa klabu utafanikisha usajili wowote mkubwa au kama Zirkzee ataendelea kubaki kikosini.