Manchester United yajipanga kumbakiza nyota chipukizi JJ Gabriel
Jitihada za dakika za mwisho za Man Utd
Klabu ya Manchester United imeamua kuingilia kati sakata la mchezaji chipukizi JJ Gabriel, ambaye amedai kutaka kuondoka klabuni hapo mara moja. Habari zilizothibitishwa na mchambuzi wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, zinaeleza kuwa viongozi wa juu wa klabu hiyo wamepanga kufanya mazungumzo na kijana huyo mwenye umri wa miaka 15 ili kujaribu kurekebisha hali hiyo.
Inaelezwa kuwa Sir Jim Ratcliffe, ambaye ni mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo, amejihusisha moja kwa moja katika jitihada hizi za kuhakikisha kuwa mmoja wa vipaji bora zaidi vilivyopata kutokea katika akademi yao hakiondoki. United inamtazama Gabriel kama mchezaji mwenye mustakabali mkubwa sana na hawapo tayari kumpoteza kirahisi.
Hali ni tete
Ingawa klabu inataka kumbakiza, hali bado ni ngumu. Gabriel na wawakilishi wake wamechukua hatua kali ya kuandika barua rasmi ya kutaka kuvunja mkataba wake na ameacha kufanya mazoezi na timu hiyo. Romano anabainisha kuwa klabu haitaki kumlazimisha yeyote kubaki kwa nguvu, bali wanataka kutumia mazungumzo ili kuona kama kuna mwanya wa maelewano.
“Manchester United haijakata tamaa. Wanatambua kuwa ni kazi ngumu, lakini wapo tayari kufanya mazungumzo na familia ya mchezaji pamoja na mawakala wake ili kuona kama wanaweza kuweka mambo sawa,” alisema Romano.
Real Madrid mbele katika mbio za kumsajili
Licha ya United kung’ang’ania, klabu kubwa barani Ulaya zimeshaanza kumuwania kijana huyo. Kwa sasa, klabu ya Real Madrid inaonekana kupewa nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa kumsajili Gabriel iwapo ataondoka Old Trafford.
Barcelona pia inatajwa kuwa katika mawasiliano, huku klabu nyingine kubwa kama Bayern Munich na Paris Saint-Germain zikifuatilia kwa karibu maendeleo ya sakata hili. Hapo awali, Manchester City ilikuwa imefikia hatua za mwisho kumsajili kijana huyo mwaka mmoja uliopita kabla hajabadili uamuzi na kubaki Manchester United.
Kwasasa, uamuzi wa mwisho utategemea zaidi familia ya Gabriel na njia watakayoona inafaa kwa maendeleo ya kipaji chake. Dunia ya soka inasubiri kuona kama mazungumzo ya Sir Jim Ratcliffe yatazaa matunda au kama kijana huyo atatimkia Hispania.