Manchester United yajipanga kutoa ofa nono kwa Warren Zaire-Emery
United yatafuta kiungo mwingine
Manchester United inaendelea na mikakati yake ya kuimarisha safu ya kiungo kuelekea msimu ujao, huku ripoti mpya zikieleza kuwa klabu hiyo inajiandaa kuweka mezani ofa ya euro milioni 60 (takriban pauni milioni 51) kwa ajili ya kiungo wa Paris Saint-Germain, Warren Zaire-Emery.
Hadi sasa, mashetani wekundu hao tayari wamefanikiwa kuwasajili Andrey Santos kutoka Chelsea na Youri Tielemans kutoka Aston Villa. Hata hivyo, kocha Michael Carrick anaonekana bado anahitaji nyongeza ya kiungo mwingine mmoja, pamoja na mchezaji wa pembeni na beki, ili kuifanya timu hiyo iwe na ushindani wa kweli katika mashindano yote watakayoshiriki.
Changamoto za usajili
Awali, United ilikuwa katika hatua za mwisho kumsajili kiungo Ederson kutoka Atalanta, lakini dili hilo lilikwama dakika za mwisho baada ya majibu ya vipimo vya afya kuibua hofu juu ya tatizo la goti kwa mchezaji huyo. Hii ndiyo sababu iliyoifanya klabu kuanza kutazama njia mbadala.
Majina mengi yamehusishwa na United hivi karibuni, ikiwemo Manu Kone wa Roma, Alex Scott wa Bournemouth, na Aurelien Tchouameni wa Real Madrid. Sasa, kijana wa PSG, Warren Zaire-Emery, amejitokeza kama shabaha mpya ambayo klabu inataka kuijaribu.
Je, ni lengo halisi au ndoto tu?
Licha ya ripoti za maandalizi ya ofa hiyo, wachambuzi wa mambo wanaonekana kuwa na mashaka. Mwandishi maarufu wa habari za usajili, Fabrizio Romano, ameweka wazi kuwa usajili wa Zaire-Emery unaonekana kuwa “ndoto” zaidi kuliko uhalisia kwa wakati huu.
“Tumeona taarifa nyingi zikimhusisha Warren Zaire-Emery na Manchester United, lakini kwa uelewa wangu, Paris Saint-Germain hawana mpango wowote wa kufanya mabadiliko katika safu yao ya kiungo kwa sasa. Wameridhishwa sana na kikosi walichonacho,” alisema Romano kupitia chaneli yake ya YouTube.
Romano aliongeza kuwa PSG wamejipa uhakika zaidi baada ya kumpa mkataba mpya Fabian Ruiz. Kwa sasa, PSG wanatathmini thamani ya Zaire-Emery kuwa karibu euro milioni 80, jambo linalofanya ofa ya United ionekane kuwa ndogo sana kwa klabu hiyo ya Ufaransa, huku wakiwa hawana haraka ya kumuuuza kiungo huyo mwenye umri wa miaka 20.