Manchester United yafanya kweli, yanyakua vipaji kutoka Liverpool na Man City
United yajenga msingi imara kwa kusajili vijana
Manchester United imeendelea na mkakati wake wa kuimarisha akademia ya klabu hiyo kwa kufanya usajili wa kushtukiza kutoka kwa wapinzani wao wakubwa kwenye Ligi Kuu ya England. Klabu hiyo imefanikiwa kumpata winga kinda Isaac Konde akitokea Liverpool na kiungo Karim Cassim kutoka Manchester City.
Uhamisho wa Isaac Konde, kijana mwenye umri wa miaka 16, unatajwa kuwa pigo kubwa kwa Liverpool kutokana na kipaji kikubwa alichonacho kinda huyo. Ripoti kutoka kwa mwandishi Andy Mitten zinaeleza kuwa mazungumzo kuhusu kifuta jasho kati ya klabu hizo mbili yanaendelea, huku mchezaji huyo tayari akiwa amesaini mkataba wa kujiunga na Old Trafford.
Mchezaji mwenye sifa za Nani na Zaha
Konde anatarajiwa kuanza maisha yake United kwa mkataba wa masomo wa mwaka mmoja, kabla ya kuingia kwenye mkataba wa kitaalamu wa miaka mitano. Atakuwa chini ya uangalizi wa Darren Fletcher katika kikosi cha vijana cha chini ya miaka 18 (U-18).
Kocha mmoja aliyewahi kufanya kazi na kinda huyo amemwelezea kama mchezaji mwenye kasi na uwezo wa kipekee wa kucheza pembeni, akimfananisha na mastaa wa zamani wa United, Nani na Wilfried Zaha.
“Ana kasi, anapenda kushambulia moja kwa moja na ni mchezaji mwenye kusisimua. Ananikumbusha sana Nani au Wilfried Zaha. Ana kila sifa ya kuwa mchezaji wa Manchester United,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo, mashabiki wametakiwa kuwa na subira kwani mchezaji huyo bado anahitaji muda wa kurejea kwenye hali yake ya kawaida ya kimchezo na kuimarisha mwili wake kabla ya kuonyesha uwezo wake kamili.
Karim Cassim ajiunga pia
Siku moja tu baada ya kumpata Konde, United ilithibitisha kumsajili kiungo Karim Cassim mwenye umri wa miaka 17 kutoka Manchester City. Cassim, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya England, alikuwa sehemu ya kikosi cha City kilichotwaa taji la FA Youth Cup msimu uliopita.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa na klabu, Manchester United imemkaribisha kijana huyo huku ikionyesha imani kubwa na uwezo wake wa kuendeleza kipaji chake ndani ya viunga vya Old Trafford. Usajili huu unaonekana kama sehemu ya mpango mpana wa kocha Michael Carrick wa kujenga kizazi kipya kitakachosaidia kurejesha heshima ya klabu hiyo.