Carlos Baleba anatajwa kuwa suluhisho la kiungo pale Manchester United
United yatafakari njia mbadala
Baada ya kupoteza nafasi ya kuwanasa viungo kadhaa waliokuwa kwenye rada zao, Manchester United sasa inatajwa kuangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Brighton, Carlos Baleba. Hii inakuja baada ya klabu hiyo kushindwa kufikia makubaliano ya kifedha kwa ajili ya wachezaji wengine wengi katika kipindi hiki cha usajili.
Awali, United ilihusishwa na viungo kama Elliot Anderson, Mateus Fernandes, na Sandro Tonali, lakini masuala ya gharama za uhamisho yalikwamisha mipango hiyo, na hatimaye baadhi ya nyota hao kutua klabu nyingine.
Baleba ni chaguo la wazi
Mwandishi wa habari za michezo, Ben Jacobs, amebainisha kuwa mlango uko wazi kwa United kumsajili Baleba, ikiwa tu wataamua kuweka mkazo kwenye mazungumzo na Brighton. Inafahamika kuwa tayari kulishakuwa na makubaliano ya awali ya maslahi binafsi kati ya mchezaji huyo na United tangu msimu uliopita.
“Ninahisi wana malengo mengine mbele ya Baleba. Lakini huu ni usajili ambao hawaitaji kuupa kipaumbele kikubwa kama wengine, kwa sababu mchezaji mwenyewe anataka kujiunga na Man Utd na tayari kulikuwa na makubaliano mepesi ya kibinafsi tangu msimu uliopita,” alisema Jacobs kupitia The United Stand.
Changamoto ya bei
Licha ya Baleba kuonyesha nia ya kutaka kujiunga na wababe hao wa Old Trafford, kikwazo kikubwa bado ni bei anayotajwa kuuzwa na klabu yake ya Brighton. Msimu uliopita, Brighton iliweka dau la pauni milioni 100 kwa ajili ya kiungo huyo, jambo ambalo lilivunja mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Ripoti kutoka Manchester Evening News zinaeleza kuwa, licha ya Baleba kutokuwa na msimu mzuri sana kule Sussex, Brighton bado haijaonyesha dalili za kushusha bei ya mchezaji huyo kutokana na hali ya soko la sasa la wachezaji wa nafasi ya kiungo kuwa na bei ya juu.
Uamuzi uko mikononi mwa United
Kufikia sasa, United haijaonyesha haraka yoyote ya kumalizana na Brighton kwa ajili ya Baleba, ingawa anatajwa kama mmoja wa wachezaji sita walio kwenye rada za klabu hiyo kwa ajili ya kuimarisha safu ya kiungo. Hata hivyo, ikitokea United ikashindwa kupata saini za malengo yao mengine na hali ya uhitaji ikaongezeka, Baleba anabaki kuwa chaguo ambalo linaweza kufanyika ikiwa klabu hiyo itakuwa tayari kufungua pochi zao.
Kwa sasa, mashabiki wa United wanaendelea kusubiri kuona ni hatua gani klabu itachukua katika siku hizi za dirisha la usajili ili kuimarisha kikosi chao.