Manchester United yataja majina mawili mapya ya viungo wanaowataka
Utafutaji wa viungo unaendelea Old Trafford
Manchester United inaendelea na pilikapilika za kusaka viungo wapya kwenye dirisha hili la usajili ili kuimarisha kikosi cha kocha Michael Carrick. Baada ya kupoteza nafasi za kusajili baadhi ya malengo yao ya awali, sasa klabu hiyo imeanza kutazama chaguzi nyingine muhimu.
Mwandishi maarufu wa habari za usajili, Fabrizio Romano, amebainisha kuwa mabingwa hao wa kihistoria wanawatazama kwa umakini Aurelien Tchouameni wa Real Madrid na Alex Scott anayekipiga Bournemouth. Hatua hii inakuja wakati klabu hiyo ikihitaji zaidi viungo baada ya kuondoka kwa Casemiro na majeraha ya muda mrefu ya Manuel Ugarte.
Changamoto kwenye usajili
United tayari ina makubaliano na Atalanta kwa ajili ya kumsajili Ederson Silva, lakini uongozi wa INEOS unaamini kuwa wanahitaji angalau kiungo mwingine mmoja au wawili ili kuwa na kikosi kipana kuelekea msimu mpya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (Champions League).
Awali, United ilikuwa inawafuatilia Elliot Anderson, Sandro Tonali, na Mateus Fernandes, lakini mipango hiyo haikufanikiwa. Anderson alijiunga na Manchester City, Fernandes akaelekea Tottenham Hotspur, huku Tonali naye akitajwa kuwa njiani kujiunga na Spurs akitokea Newcastle.
Tchouameni na Scott wanavyotazamwa
Akizungumzia hali hiyo, Romano alieleza kuwa United inawaona Tchouameni na Scott kama wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuwasaidia.
“Majina mawili ambayo Manchester United wanayachukulia ndani ya klabu kama machaguo bora ni Aurelien Tchouameni, ingawa tatizo ni mshahara wake na kwa sasa Real Madrid hawajatoa ruhusa ya kumuuza, na pia Alex Scott ambaye anathaminiwa sana na Arsenal pamoja na United.”
Kwa upande wa Alex Scott, Bournemouth wamekuwa wakisisitiza kuwa hawapo tayari kumwachia kiungo huyo na hata wamepanga kumpa mkataba mpya. Hata hivyo, hali inaweza kubadilika endapo ofa nono itawasilishwa kwenye meza ya mazungumzo.
Kwa sasa, mashabiki wa United wanabaki kusubiri kuona ni nani atatua Old Trafford, kwani klabu hiyo inahitaji haraka kuziba pengo la viungo wake kabla ya msimu kuanza.