Manchester United yafukuzia saini ya nyota wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly
United yataka kuimarisha eneo la beki na kiungo
Manchester United inaendelea na pilikapilika za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao, na safari hii taarifa zimeibuka kuwa klabu hiyo inamnyatia nyota wa Arsenal, Myles Lewis-Skelly.
Klabu hiyo inayomilikiwa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya INEOS, inaelezwa kuwa na nia ya kufanya jaribio la kushtukiza kumpata mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kushoto na kiungo. Utofauti huu wa kucheza nafasi nyingi umemvutia kocha Michael Carrick anayetafuta mbadala sahihi wa Luke Shaw.
Hali ya mambo ndani ya Arsenal
Ripoti zinaeleza kuwa United wanachunguza kama Arsenal wako tayari kumwachia kinda huyo, hasa ikizingatiwa kuwa timu hiyo ya Mikel Arteta inahusishwa na mipango ya kuwasajili wachezaji wakubwa kama Bruno Guimaraes kutoka Newcastle na Vinicius Junior kutoka Real Madrid.
Ikiwa Arsenal itafanikiwa kupata saini za nyota hao, inadhaniwa kuwa mabadiliko ya mfumo wa timu yanaweza kumlazimu Lewis-Skelly kufikiria upya hatima yake. Hata hivyo, taarifa zinaweka wazi kuwa kwa sasa Arsenal hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo kama kipaumbele chao cha sokoni.
Lewis Hall naye yumo kwenye rada
Sambamba na Lewis-Skelly, Manchester United pia inamfukuzia beki wa Newcastle United, Lewis Hall. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Uingereza na anafanana na Lewis-Skelly kwa uwezo wake wa kucheza beki na kiungo.
Kulingana na mwandishi wa habari za Manchester United, Andy Mitten, inafahamika kuwa Hall mwenyewe ana hamu kubwa ya kutua Old Trafford.
“Wanamvutia Lewis Hall wa Newcastle United, lakini Newcastle watahitaji pesa nyingi kwa ajili yake, hivyo si jambo rahisi kama kufanya maamuzi na kununua tu. Nina uhakika mchezaji anataka kujiunga na Man Utd, lakini si yeye tu anayeamua, bado ana mkataba na klabu nyingine.”
Kwa sasa, Manchester United inaonekana kuelekeza nguvu zake katika kuhakikisha wanasuka upya safu ya ulinzi na viungo kabla ya dirisha la usajili kufungwa, huku mashabiki wakisubiri kuona ni nani kati ya walengwa hao atakayewasili klabuni hapo.