Skip to content

Roberto Mancini afunguka kuhusu mkataba tata Manchester City

SokaNews
Updated: Published: Jumatatu, 28 Septemba 2026 · 2 min read
manchestercity robertomancini premierleague fedha sokalauingereza
Roberto Mancini afunguka kuhusu mkataba tata Manchester City

Uvumi wa mkataba tata

Kocha wa zamani wa Manchester City, Roberto Mancini, amezua mjadala mzito baada ya kukiri hadharani kuwa alikuwa na kile kinachoitwa ‘mkataba pacha’ (double contract) wakati akinoa miamba hiyo ya Etihad. Kauli hii inakuja wakati Manchester City ikiwa kwenye wakati mgumu baada ya kubainika kukiuka sheria za kifedha za Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League).

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, klabu hiyo imekutwa na hatia ya kukiuka takriban mashtaka 115 yaliyowasilishwa na bodi ya ligi. Moja ya tuhuma hizo nzito ni kushindwa kuweka wazi malipo sahihi ya wachezaji na makocha kati ya mwaka 2009 na 2018. Gazeti la Der Spiegel la nchini Ujerumani liliwahi kuchapisha nyaraka zikionyesha kuwa mshahara wa msingi wa Mancini ulikuwa £1.45m, lakini ukaongezwa maradufu kupitia mkataba mwingine wa ushauri na klabu moja ya Abu Dhabi.

Majibu ya Mancini

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari nchini Italia kuelekea mchezo wa Nations League dhidi ya Uturuki, kocha huyo ambaye aliiongoza City kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa ligi mwaka 2012, alionekana kutotaka kuhusishwa na sakata hilo.

“Sio tatizo linalonihusu mimi. Hata hivyo, sio kitu kipya kwa sababu kila baada ya miaka minne au mitano jambo hili hurejewa. Manchester City haina hatia, na suala la kuwa na mkataba wa pili sio tatizo langu, labda ni lao,” alisema Mancini.

Msimamo wa City na hofu ya adhabu

Licha ya presha hiyo kubwa, uongozi wa Manchester City kupitia mwenyekiti wao, Khaldoon Al Mubarek, umesisitiza kuwa klabu hiyo haina hatia na iko tayari kupambana kisheria ili kuthibitisha ukweli. Katika barua iliyoandikwa kwa mashabiki, klabu hiyo ilieleza kuwa mchakato wa kisheria bado ni mrefu na wana imani kubwa ya kushinda kesi hiyo.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya soka wameonya kuwa hali inaweza kuwa mbaya kwa ‘Citizens’ ikiwa watapatikana na hatia ya kudumu. Mwandishi Ben Jacobs amedai kuwa uongozi wa Premier League unashinikiza adhabu kali, ikijumuisha kupokwa pointi nyingi au hata kushushwa daraja moja kwa moja.

Kuna taarifa pia zinazodai kuwa ikiwa Manchester City itafukuzwa kutoka Ligi Kuu ya Uingereza, hata ligi za chini (EFL) zinaweza kutokuwa tayari kuwapokea, jambo linaloleta hofu ya ‘mwisho wa dunia’ kwa klabu hiyo yenye maskani yake jijini Manchester.